kashfa zazidi kumuandama Trump
17 Mei 2017Ikulu ya Marekani ya White House ilikana vikali baada ya dondoo hizo kuwekwa wazi baadaye jana, mwishoni mwa siku iliyokuwa na heka heka nyingi za kupambana na ripoti zilizoonekana kuwa na madhara makubwa tangu mapema kwa utawala huo.
Taarifa hizo kutoka kwa James Comey zimekuja wakati utawala huo uliojiingiza katika matatizo ulikuwa bado unahangaika kutoa maelezo kuhusu taarifa zilizojitokeza kwamba rais alitoa taarifa nyeti kwa waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi pamoja na balozi wa nchi hiyo nchini Marekani. Wakitetea hatua za Trump , maafisa walipuuzia umuhimu na usiri wa taarifa hizo, ambazo ziliwasilishwa na Israel chini ya makubaliano ya kubadilisha taarifa za kijasusi, na Trump binafsi amesema ana haki zote, kama rais kubadilishana taarifa hizo zinazohusu ugaidi na usalama wa safari za anga na Urusi.
Pamoja na hayo washirika wa Marekani na baadhi ya wajumbe wa baraza la Congress wameeleza wasi wasi wao unaokaribia kuwa tahadhari. Seneta kutoka chama cha Republican John McCain ametoa matamshi makali jana kuwahi kutolewa na kambi ya chama cha Republican. Licha ya kwamba hata baada ya jana kutolewa taarifa hiyo, wajumbe kutoka chama hicho walisita kumkosoa rais, licha ya kwamba mbinyo wa kujitokeza kufanya hivyo ukiongezeka. McCain amesema hali hii sasa imekaribia kiwango cha kashfa kubwa ya Watergate.
"Kitu ninachoweza kusema ni kwamba tuliisha ona filamu hii hapo kabla. Nafikiri inafikia katika kiwango ambapo ni sawa na Watergate na viwango vya kashfa nyingine ambazo mimi na wewe tumekwisha shuhudia. Ni kama jongoo mwenye miguu mingi , na kwamba kila mara kiatu kikitoka mguuni kila baada ya siku kunaonekana upande mwingine wa hali hii isiyofurahisha."
Kwa upande wa Comey binafsi ambaye Trump alimfuta kazi wiki iliyopita, mkurugenzi huyo wa shirika la FBI aliandika katika kumbukumbu baada ya mkutano wa mwezi Februari katika Ikulu ya White House kwamba rais mpya amemuomba kufunga uchunguizi wa shirika hilo kumhusu Flynn na mawasiliano yake na Urusi, amesema mtu aliyesoma kumbukumbu hizo. Uchunguzi kuhusu Flynn ulikuwa sehemu ya uchunguzi mpana zaidi kuhusiana na Urusi kuingia uchaguzi wa rais mwaka jana.
Mbunge wa baraza la wawakilishi Jason Chaffetz , mwenyekiti wa kamati ya bunge kutoka chama cha Republican , ametuma barua kwa shirika la FBI jana Jumanne inayoomba kwamba shirika hilo liwasilishe nyaraka zote na sauti zote zilizorekodiwa ambazo zinaeleza kuhusu mawasiliano kati ya Comey na Trump. Amesema anaipa shirika la FBI wiki moja na kama tutahitaji kushitaki tutafanya hivyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Yusuf Saumu