Katiba yamfungulia njia al-Sisi, lakini vijana wajitenga
20 Januari 2014Wapiga kura waliipitisha katiba hiyo wiki iliyopita kwa asilimia 98.1, na matokeo yake yanaonekana kama ishara ya ndiyo kwa Jenerali Abdel-Fattah al- isi kugombea urais. Sisi aliongoza njama za kumuangusha rais Mohammad Mursi mwezi Julai, kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake wa mwaka mmoja, ambao ulikuja baada ya maandamano yaliyomuangusha mtangulizi wake Hosni Mubarak mwaka 2011.
Hofu ya kurudi kwa udikteta
Makundi ya vijana yaliyokuwa msitari wa mbele katika maandamano yaliyohitimisha tawala za Mursi na Mubarak, hawakupinga wakati serikali iliyowekwa na jeshi ilipofanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya wafuasi wa Mursi. Na wala hawakupinga pale kundi la Mursi la udugu wa Kiislamu lilipopigwa marufuku na kutajwa kuwa ni kundi la kigaidi.
Lakini walielezea kughadhabishwa baada ya serikali inayoungwa mkono na jeshi kupitisha sheria mwezi Novemba, ambayo inapiga marufuku maandamano yasiyoidhinishwa. Na hili lilionekana kuakisiwa wazi wakati wa zoezi la kupiga kura. Sisi aliwasihi vijana kushiriki katika kura ya maoni, akisema wanachangia zaidi ya asilimia 50 ya raia milioni 85 wa nchi hiyo.
Lakini waandishi wa habari wa shirika la AFP waliotembelea vituo vya kupigia kura walisema vijana hawakushiriki zoezi hilo kwa nguvu, na wachambuzi walithibitisha kuwa vijana wengi wanaopigania mabadiliko wajitenga na kura hiyo.
Mchambuzi wa kisiasa Hassan Nafea alisema mwitikio wa kura hiyo ulikuwa unakatisha tamaa. Nafea alisema vijana walikataa kushiriki kura ya maoni kwa sababu wanachukulia mambo yanayofanyika hivi sasa kama mapinduzi dhidi ya mapinduzi ya Januari.
Mkuu wa tume ya uchaguzi Nabil Salib alitangaza matokeo siku ya Jumamosi na kusema kuwa ushiriki ulifikia asilimia 38.6 ya wapiga kura milioni 53, ambapo ni asilimia 1.9 tu waliopiga kura ya Hapana. Salib alisema asilimia fulani ya vijana hawakushiriki kwa sababu kura hiyo ilifanyika wakati wa mitihani, vinginevyo mwitikio ungekuwa mkubwa zaidi.
Udugu wa Kiislamu wapinga
Lakini kundi la Udugu wa Kiislamu lilisema katika taarifa kuwa wapiga kura vijana hawakuwa wanashughulishwa na mitihani, bali walikuwa wanashghulishwa na maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi na kura ya maoni isiyo halali.
Lakini Nafea alisema matokeo ya kura hiyo yalionyesha kuungwa mkono kwa Sisi kugombea urais, kwa sababu ya kile alichosema kuwa sehemu kubwa ya Wamisri wanauona Udugu wa Kiislamu kama kitisho kwa jamii.
Sisi amesema huenda akagombea urais ikiwa ataombwa kufanya hivyo. Jenerali huyo anapendwa na mamilioni waliyoingia mitaani dhidi ya Mursi, lakini wafuasi wa udugu wa Kiislamu wanamlaani kwa kile wanachosema ni mapinduzi dhidi ya rais wa kwanza aliechaguliwa kidemokrasia nchini Misri.
Udugu wa Kiislamu, ambao umekumbana na ukandamizaji mbaya kutoka kwa serikali na kuuawa kwa wafuasi wake zaidi ya 1,000, umeipuuza kura ya maoni kama kichekesho. Vijana wengi wanakubaliana, lakini kwa sababu tofauti.
Watenda kinyume na wasemavyo
Mohamed Ghorab kutoka kundi linalopinga raia kushtakiwa na makahama za kijeshi, alisema kwao ni jambo la kushangaza kuwa katiba hiyo inazungumzia uhuru wa kujieleza wakati wale walioipinga katiba hiyo wamefungwa jela.
Alisema kwa wengi huo ni ukumbusho wa enzi za utawala wa Mubarak. Viongozi maarufu wa vijana kutoka mapinduzi ya mwaka 2011 dhidi ya Mubarak wamefungwa katika wiki za hivi karibuni. Miongoni mwao ni Ahmed Maher, Ahmed Douma na Mohamed Adel, ambao walikutikana na hatia mwezi Desemba kwa kuandaa maandsmano yasiyoruhusiwa.
Kesi hizi zimelaaniwa na makundi ya haki za binaadamu na wataalamu wanaosema zinatishia mafanikio yaliyopatikana tangu kuondolewa kwa Mubarak, na ishara ya kurejea katika utawala wa kidikteta.
Siku ya Jumapili, katika jaribio la kuwapooza vijana, rais wa muda Adly Mansour alisema vijana ndiyo walikuwa Ingini ya mapinduzi yote, na kuongeza kuwa mchango wao bado haujaisha, na kuwataka washiriki mchakato wa kisiasa, kwa vile uhuru sasa umehakikishwa.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman