Katibu Mkuu wa chama tawala Tanzania ajiuzulu
30 Novemba 2023CCM imesema imeridhia kuondoka kwa mtendaji huyo, huku ikieleza kuwa imeanzisha uchunguzi kubaini kiini kilichoko nyuma yake mpaka kiongozi huyo kuamua kuachia ngazi katika maamuzi ya ghafla.
"Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, aliuarufu mkutano wa Kamati Kuu, NEC, kwamba alipokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa Katibu Mkuu na kwamba ameridhia maombi yake," Katibu wa Itakadi na Uenezi wa CCM Paul Makonda aliuambia mkutano wa habari baada ya kikao cha NEC.
Chongolo ambaye alichukuwa nafasi ya katibu mkuu baada ya mtangulizi wake, Dr Bashir Ally kuondolewa, amechukua uamuzi usiotarajiwa na wengi na ambao unaanzisha maswali na mjadala mpya kuhusu kile kinachoendelea ndani ya chama hicho ambacho kimeanza kujiweka mguu sawa kuelekea katika uchaguzi ujao.
CCM kuchunguza sababu za kujizulu kwake
Makonda hakufafanua sababu za kujiuzulu kwa Chongolo, ambaye aliteuliwa Katibu Mkuu wa CCM Aprili 2021. Lakini CCM imesema itaanzisha uchunguzi kubaini sababu za hatua hiyo.
Soma pia: CCM yabariki uwekezaji bandari nchini Tanzania
Katika barua aliomuandikia mwenyekiti wa chama na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Chongo alizungumzia sababu za kuchafuliwa jina lake kwa kuhusishwa na mambo ambayo hakuyataja wazi wazi.
"Chama cha Mapinduzi kikiwa na utulivu basi na siasa za Tanzania zitakuwa na utulivu kwa hiyo mimi naweza kusema kilichotokea ni sawa sawa na kipindi kile ambapo Mzee Jumbe alitakiwa kujiuzulu nafasi zote za chama na serikali kwa sababu ya kuchafuka kwa hali ya hewa," alisema Hafidh Kido, mchambuzi na mwandishi habari.
Kuondoka kwa Chongolo ambaye pia kitaaluma ni mwandishi wa habari, huenda kukaanzisha vikumbo vipya vya kuwania nafasi yake, ingawa kwa wakati huu, kulingana na katibu wa uenezi wa chama hicho, Paul Makonda nafasi yake itashikwa kwa muda na naibu katibu mkuu, Anamringi Macha.
Maandalizi kuelekea uchaguzi
Wachambuzi wa mambo wanaendelea kuyatazama kwa jicho la karibu hayo yanayoendelea kujitokeza ndani ya chama hicho hasa wakati huu ambako wanasiasa wameanza kujipanga kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu wa mwaka 2025.
Soma pia: Rais Samia Suluhu akutana na vyama vya siasa
Kuhusu hatma ya chama hicho kulekea katika chaguzi hizo, Mchambuzi wa Eric Bernard anasema huenda CCM inajipanda kwenda kwenye uchaguzi mkuu ikiwa na mtendaji mkuu wa chama mwenye uzoefu na anaekijua vyema chama.
CCM haijaweka bayana muda gani itatumia kukamilisha uchunguzi wake kubaini mazingira yaliyosababisha kujiuzulu kwa mtendaji wake lakini imesisitiza kuweka wazi uchunguzi wake.