Kenya bingwa CECAFA, Zanzibar mashujaa
18 Desemba 2017Kenya imeshinda kombe la Challenge la shirikisho la vyama vya kandanda Afrika mashariki na kati Cecafa jana Jumapili wakati walipoishinda Zanzibar Heroes kwa mabao 3-2 katika mikwaju ya penalti kufuatia sare ya mabao 2-2 hadi mchezo kumalizika kwa dakika za nyongeza mjini Machakos nchini Kenya.
Ovella Ochieng aliipatia wenyeji Kenya bao la kuongoza katika dakika ya tano ya mchezo, lakini Zanzibar wakiwania ubingwa wao wa kwanza tangu miaka 22 iliyopita, ilisawazisha katika dakika ya 87 kwa bao la khamis Mussa. Kenya ilipata bao tena la kuongoza dakika saba katika kipindi cha kwanza cha nyongeza wakati Masood Juma alipotumia makosa ya mlinda mlango wa Zanzibar, lakini Zanzibar Heroes walirejesha bao hilo kwa bao tena la Mussa na kusababisha mchezo huo kuamuliwa bkwa mikwaju ya penalti.
Mlinda mlango wa Kenya Patrick Matasi alikuwa nyota katika mikwaju ya penalti akiokoa mikwaju mitatu na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.
Timu ya taifa ya Zanzibar Zanzibar Heroes ilipokelewa kwa shangwe kama mashujaa wa kweli mjini Zanzibar leo mjini Unguja.
Mwaka 1995 Zanzibar kwa mara ya kwanza ilifanikiwa kunyakua kombe hilo lakini limekuwa ndoto tangu wakati huo na mwaka huu timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes imeshangaza kila shabiki wa kandanda katika Afrika mashariki na kati pale ilipoanza kwa kuiangusha Rwanda kwa mabao 3-1 na kisha kuikandika Tanzania bara kwa mabao 2-1 na pia Uganda mabingwa watetezi wa kombe hilo linaloshindaniwa kila mwaka kwa mabao 2-1 pia.
Nilizungumza na mchambuzi wa masuala ya kandanda wa DW na ambaye hivi sasa yuko Zanzibar kwa mapumziko Ramadhan Ali , ambaye pia aliwahi kuichezea timu hiyo ya taifa Zanzibar Heroes katika miaka ya 60 wakati wa kombe la Gossege. Nilimuuliza kuhusu historia ya Zanzibar kucharuka na mara kurudi nyuma katika kandanda la Afrika mashariki na kati.
Ni mara ya saba Kenya kunyakua kombe hilo, mara hii kwa uongozi wa kocha mpya Paul Put akipata mafanikio yake ya kwanza tangu alipoanza kuifunza timu hiyo ya taifa mwezi uliopita. Mabingwa wa zamani Uganda waliishinda Burundi kwa mabao 2-1 na kushika nafasi ya tatu.
Bundesliga
Kwa upande wa Bundesliga ligi kuu hapa Ujerumani , mwishoni mwa juma ilitimiza mchezo wake wa 17 , na kwa kawaida unakuwa mchezo wa mwisho katika duru ya kwanza ya msimu. Bundesliga inakwenda mapumziko hadi tarehe 12 Januari 2018 ambapo ligi hiyo itarejea tena viwanjani ambapo Leverkusen itakuwa mwenyeji wa FC Bayern Munich.
Hadi katika mchezo huo wa 17, Bayern Munich inaongoza kwa kuwa na pointi 41 , ikiwa mbele kwa pointi 11 kutoka timu inayoifuata Schalke 04 ambayo ina pointi 30 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Eintracht Frankfurt siku ya Jumamosi. RB Leipzig iliyokuwa ikishikilia nafasi ya pili imeporomoka hadi nafasi ya 5 baada ya kukandikwa mabao 3-2 na Hertha Berlin jana Jumapili.
Borussia Dortmund ambayo iliachana na kocha wake Peter Bosz, na kumpa kazi hiyo Peter Stoeger ilizinduka katika michezo miwili ya mwisho na kupata ushindi ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 siku ya Jumamosi dhidi ya Hoffenheim. BVB inashika sasa nafasi ya 3 ikiwa na pointi 28.
Mabao manane yalitinga nyavuni jana Jumapili katika pambano kati ya Hannover dhidi ya Bayer Leverkusen ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 4-4 na Leverkusen kupoteza fursa ya kuchupa hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na kubakia katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 28 nyuma ya Borussia Dortmund.
Kombe la DFB
Lakini kabla mwaka haujamalizika kuna patashika nyingine inatarajiwa siku ya Jumatano wakati Bayern Munich itakapopambana na Borussia Dortmund katika mchezo wa kufunga mwaka wa kombe la shirikisho , DFB Pokal. ushindi mara mbili mfululizo wa kocha mpya Peter Stoeger umeiamsha Dortmund katika mzingizi mzito wa majira ya baridi na inakumbana na Bayern Munich siku ya Jumatano ikiwa na hali mpya ya kujiamini.
Mainz na VFB Stuttgart zitaanza kuwania nafsi ya kucheza katika robo fainali ya kombe la shirikisho kesho Jumanne, ambapo pia schalke 04 itakwaana na FC Kolon ambayo ilipata ushindi wake wa kwanza katika Bundesliga msimu huu baada ya kuiangusha Wolfsburg kwa bao 1-0.
Nuerenburg itawakaribisha VFL Wolfsburg katika mchezo mwingine na Ingolstadt itakuwa wageni wa Parderborn.
Siku ya Jumatano Bremen itaumana na freiburg katika pambano la timu za ligi daraja la kwanza Bundesliga , Gladbach itaikaribisha Leverkusen na Heidenheim itakuwa wenyeji wa Frankfurt.
Katika ligi ya England , Premier League , Kocha Jurgen Klopp anakiri kwamba Manchester City haitakuwa rahisi kuikamata , lakini kocha huyo wa Liverpool atafurahi iwapo ataweza hata kunyakua nafasi moja kati ya nne za juu.
Liverpool iliishinda Bournemouth kwa mabao 4-0 na kujiweka katika nafasi ya nne , pointi 4 nyuma ya Chelsea iliyoko katika nafasi ya tatu . Lakini kocha wa Manchester United mahasimu wakubwa wa Manchester City Jose Mourinho amesisitiza kuwa timu yake haitakata tamaa katika kinyang'anyiro cha kuwania taji la ligi hiyo baada ya pointi za uongozi za Manchester punguzwa hadi pointi 11 na Machester United iliyoko katika nafasi ya pili. Kikosi cha Jose Mourinho kiliishinda West Bromwich jana Jumapili kwa mabao 2-1.
Wakati huo huo Manchester City itafanya mazungumzo na kocha Pep Guardiola mwishoni mwa msimu kuhusu kuongeza mkataba wake kwa miaka mitatu, vimesema vyombo vya habari vya Uingereza.
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil Kaka ametangaza kwamba anatundika madaluga juu na kufikisha mwisho muda wake wa kucheza soka ya kulipwa, jana akidokeza kwamba huenda akaamua kuingia katika kazi ya uongozi katika kilabu yake ya zamani AC Milan.
Mlinda mlango Peter Gulacsi amerefusha mkataba wake na RB Leipzig ya Ujerumani hadi mwaka 2022, imesema klabu hiyo ya Bundesliga jana Jumapili.
Wakati huo huo mshambuliaji wa Borussia Dortmund raia wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang amerefusha pia mkataba wake na klabu hiyo hadi mwaka 2021 vimeripoti vyombo vya habari vya Ujerumani jana Jumapili.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Mohammed Khelef