Kenya, Djibouti kurudia kura kuwania nafasi ya baraza la UN
18 Juni 2020Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limezichagua nchi nne mpya kuwa wanachama katika Baraza la Usalama ili kuhudumu katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022. Katika uchaguzi huo ambao umefanyika mjini New York, Canada imepoteza nafasi yake nayo.
India, Mexico, Norway na Ireland zimechaguliwa kuwa wanachama ambao si wa kudumu katika baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa.
Lakini Kenya na Djibouti ambazo zilishindania nafasi ya Afrika, zilishindwa kupata theluthi mbili za kura zinazohitajika, na sasa zitalazimika kushiriki duru ya pili ya uchaguzi huo leo.
Licha ya kampeni kabambe, Canada ilishindwa tena kuwa miongoni mwa wawakilishi wa nchi za Magharibi, baada ya Ireland na Norway kutwaa ushindi, matokeo ambayo huenda yakawa pigo kwa Waziri Mkuu Justin Trudeau.
Wito watolewa Afrika kupewa viti vya kudumu katika UN
Soma pia kuhusu Umoja wa Mataifa waanzisha ujumbe wa kisiasa kusaidia Sudan
Katika Ukanda wa Asia-Pasifiki, India ambayo imekuwa ikijaribu bila mafanikio kupata nafasi katika baraza hilo ambalo limetanuliwa, ilichaguliwa baada ya kukosa mpinzani, na hivyo kupata kura 184 miongoni mwa jumla ya nchi 192 zilizoshiriki.
Matokeo hayo yanamaanisha kuwa India sasa itakuwa na China katika meza moja, siku chache tu baada ya mataifa hayo mawili kulaumiana na kukabiliana katika mpaka wanaozozania wa Himalaya. Wanajeshi 20 wa India walifariki kufuatia makabiliano hayo.
Mexico ambayo pia iligombea nafasi katika baraza hilo bila ya kuwa na mshindani, ilishinda baada ya kupata jumla ya kura 187.
Katika miaka ya nyuma, mataifa ya Afrika yamekuwa yakichagua mwakilishi wao peke yao, lakini wakati huu, waliwasilisha Kenya na Djibouti.
Soma pia kuhusu Baraza la Usalama laidhinisha muongozo kuhusu amani Libya
Kenya ilipata jumla ya kura 113 nayo Djibouti ilipata kura 78 kwenye uchaguzi huo uliofanyika mjini New York. Lakini hakuna nchi yoyote kati yao ilipata wingi wa kura unaohitajika ambao ni theluthi mbili ili kupewa nafasi hiyo.
Kenya inaungwa mkono na Umoja wa Afrika, lakini Djibouti inasema ndiyo inapaswa kuipata nafasi hiyo kwa kuwa Kenya imewahi kuiwakilisha Afrika katika miaka ya nyuma.
Kenya na Djibouti zinajipigia debe huku kila upande ukiangazia juhudi zake za kutafuta amani katika pembe ya Afrika, na pia mchango wao katika hatua mbadala za ulinzi wa amani.
Kenya imetaja sifa zake za kuwapokea wahamiaji kutoka Somalia na Sudan Kusini, pamoja na michango yake kwa mataifa hayo ambayo serikali zao si imara.
Djibouti kwa upande wake inajinadi kwa kusema ipo katika eneo zuri la kimkakati pamoja na kuhifadhi kambi za kijeshi za Ufaransa, Marekani, China na Japan, na pia mchango wake nchini Somalia.
Chanzo: AFPE