1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuiondoa miraa kwenye orodha ya dawa za kulevya

28 Oktoba 2021

Serikali ya Kenya imesema itakuwa imeiondoa miraa kwenye orodha ya dawa za kulevya, miaka mitatu kutoka sasa kwa kukosa ushahidi wa kisayansi.

https://p.dw.com/p/42Ie3
Deutschland | Mehr als eine Tonne Khat beschlagnahmt
Picha: Hauptzollamt München/dpa/picture alliance

Tayari mipangilio imeanza ya kuliongezea thamani zaidi zao hilo kwa kuutumia kutengeneza mvinyo, sharubati na wiski, kama njia mojawapo ya kulivutia soko la kimataifa. 

Ni mmea mdogo wa kijani lakini uwezo wake wa kipekee umekuwa uraibu wa mamilioni ya watu ulimwenguni, ukawa kati ya mazao ya Kenya yanayouza zaidi katika soko la kimataifa. Kufikia mwaka 2011, zao la miraa lilikuwa linaipa Kenya takriban shilingi bilioni 6.9 katika soko la kimataifa.

Marekani ilipiga marufuku miraa 2014

Hata hivyo, mwaka 2014 miraa ilipigwa marufuku Marekani na katika baadhi ya mataifa ya Ulaya, ambayo yalikuwa masoko yake makubwa, lilipoainishwa kuwa kati ya dawa sugu. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa mahangaiko ya maelfu ya wakulima na wafanyibishara waliotegemea zao hilo.

Lakini sasa serikali ya Kenya inaazimia kufufua na kuboresha biashara hii. Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i amesema wizara ya afya itafanya kazi pamoja na mamlaka ya kitaifa ya kudhibiti vileo na dawa za kulevya, NACADA, kukabiliana na sifa mbaya ya zao hilo na kuwawezesha kuweka viwango vinavyofaa.

Kenia | Drogenhandel | Fred Matiang'i
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Fred Matiang'iPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

“Kufikia miaka miwili au mitatu ijayo, tunapaswa kuacha kubishana kuhusu matumizi ya miraa na badala yake, tuzindue bidhaa mbalimbali kutokana na zao hili, kama ninavyoona kwenye mpango huu; mvinyo wa miraa, sharubati ya miraa na kadhalika. Tulenge kuona kwamba wakulima na wafanyabiashara wa miraa wana fursa na masoko zaidi, na hivyo ndivyo tunapigana na umasikini,” alifafanua Matiang'i.

Mkutano wa mmea wa miraa

Kongamano la kwanza la kisayansi kuhusu mmea wa miraa limekamilika Alhamisi jijini Nairobi, dhamira kuu ikiwa kutoa ufahamu wa umuhimu wa zao la miraa kwa afya, kijamii na kiuchumii kwa kutumia ushahidi wa kisayansi. Waziri wa Kilimo Peter Munya amesisitiza haja ya kutathmini umuhimu wa zao la miraa.

Soma zaidi: Mzozo wa uuzaji miraa kati ya Kenya na Somalia

''Swala la NACADA kuendelea kuainisha miraa kama dawa ya kulevya ilhali hakuna ushahidi wowote wa kisayansi unaodhibitisha hilo, limekuwa kikwazo kikubwa,'' alisema Munya.

Kenya inalenga masoko kama vile Djibouti, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Msumbiji, Israel na Yemen. Taasisi ya utafiti wa kitabibu nchini Kenya, KEMRI, imeeleza kwamba ripoti itatolewa ikiwa na maelezo kamili ya kemikali zilizo kwenye mmea wa miraa na manufaa yake ya kiafya, pamoja na fursa na changamoto zilizoko katika soko la zao hilo na bidhaa zake.