Kenya kutoa chanjo kwa watoto 400,000 kwa siku 100
27 Juni 2018Kenya imejiandaa kuanza kutoa chanjo kwa watoto 400,000 katika siku 100 zijazo, kupitia kampeni yake kubwa iliyozinduliwa na rais Uhuru Kenyatta hii leo jijini Nairobi.
Kampeni hiyo iliyopewa jina la 'mpango ulioharakishwa wa chanjo' unalenga kuongeza idadi ya watoto wanaopata chanjo ambayo imesalia katika kiwango cha asilimia 80, chini ya malengo ya taifa ya asilimia 90.
Rais Uhuru Kenyatta alipozungumza kwenye uzinduzi wa mpango huo utakaotoa matokeo ya haraka, ambapo pia madaktari 100 waliobobea kutoka Cuba waliagwa, alisisitizia umuhimu wa chanjo kama kipengele muhimu kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote nchini humo, katika kutekeleza malengo yake manne makuu ya maendeleo.
Aidha, Rais Kenyatta ameihimiza wizara ya afya na elimu kufanya kazi kwa karibu na serikali za kaunti, kwa kutoa kipaumbele ya chanjo kwa watoto walio katika umri wa kwenda shule, akisema ni matamanio yake kuona watoto wote wanachanjwa kabla ya kujiunga na shule.