1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Wasengwer wataka kutambuliwa kuwa wenyeji wa Embobut

Shisia Wasilwa7 Oktoba 2019

Jamii ya Wasengwer nchini Kenya wamefanya maandamano wakitaka kutambuliwa kuwa wenyeji asili wa msitu wa Embobut na kwamba hawafai kutimuliwa kwenye msitu huo

https://p.dw.com/p/3Qqf4
Kenia Nairobi | Protest der Sengwer-Gemeinschaft
Picha: DW/S. Wasilwa

Jamii hiyo iliyokuwa na waakilishi wake waliwasilisha ombi lao katika ofisi ya rais wakiandanamana na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.

Maandamano ya jamii ya Wasengwer pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu yanajiri huku serikali ikiimarisha juhudi zake za kuhifadhi vyanzo vya maji nchini Kenya. Tayari watu waliouvamia msitu wa Mau bila ya nyaraka halali wameanza kuondolewa katika msitu huo ambao ni moja ya vyanzo vikuu vya maji nchini humo.

Ijapokuwa wamekuwa wakitimuliwa kila mwaka tangu mwaka 1970 katika msitu wa Embobut, Wasengwer wamekuwa wakirejea na kujenga makazi yao. Lakini mwaka 2014, polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwatimua katika makazi yao.

Wakiwa na mavazi ya kiasili ya ngozi, Wasengwer walipita katikati ya barabara zilizoko jijini Nairobi, na kuwasilisha nyaraka zao katika afisi ya rais uhuru Kenyatta iliyoko katika jengo la Harambee. Walitembea kutoka msitu huo hadi jijini Nairobi kuwaslisha malalamiko yao. Kilio chao kimepata uungwaji mkono katika medani ya kimataifa. Evelyn Juma ni mmoja wa waandamanaji kutoka kwa jamii hii.

Waapa kurejea msituni baada ya kutimuliwa

Kwa kuwatimua wasengwer na kuwachomea makazi yao, maaskari wa kulinda msitu hukiuka magizo ya mahakama, suala ambalo sasa jamii hii inataka ufumbuzi na suluhisho la kudumu. Wenyeji hao ambao ni zaidi ya 5,000 wameapa kurejea msituni humo baada ya kutimuliwa na serikali mwka 2017 wakisema ndio makazi yao.

Kenia Nairobi | Protest der Sengwer-Gemeinschaft
Waandamanaji wa jamii ya Sengwer wakwa katika maandamano jijini NairobiPicha: DW/S. Wasilwa

Wanadai kuwa serikali haikuwashauri walipokuwa wanatimuliwa. Wanasema kuwa hatua ya serikali ya kuwatimua msituni kutawafanya wapoteza utamaduni wao na pia kusaliti mababu zao.

Mwaka uliopita Umoja wa Ulaya ulisitisha shilingi bilioni 3.6 za kusaidia katika mradi wa utunzaji wa mazingira nchini Kenya baada ya mtu mmoja wa jamii ya Sengwer kuuliwa na mlinzi wa msitu. Umoja wa Ulaya uliitaka serikali ya Kenya kusuluhisha tofauti zake na jamii ya Wasengwer kabla ya kurejelea mradi huo.