Kenya yaadhimisha miaka 50 ya Uhuru
12 Desemba 2013Tokea mwaka wa 2010 Kenya inaongozwa katika msingi wa katiba mpya ya kidemokrasi. Ustawi wa uchumi ni wa juu, unaovuka asilimia tano licha ya kasoro ya ufisadi. Na kugunduliwa hivi karibuni kwa mafuta maana yake ni ustawi zaidi kwa nchi hiyo.
Mapambano dhidi ya Al-Shabaab
Kwa sasa majeshi ya Kenya yanashiriki katika juhudi za kuleta amani nchini Somalia kama sehemu ya majeshi ya Umoja wa Afrika (AMISOM).
Kutokana na Kenya kushiriki katika juhudi hizo za kulinda amani nchini Somalia, magaidi wenye itikadi kali ya kiislamu wa Al -Shabaab wanalipiza kisasi kwa kufanya mashambulio ya kikatili mara kwa mara nchini Kenya.
Taifa la vijana
Zaidi ya asilimia 60 ya Wakenya ni watu wenye umri wa chini ya miaka 24. Tulikutana na vijana wa Kenya katika mkahawa wa internet mmojawapo katika jiji la Nairobi waliokuwa wanayatafakari maendeleo ya nchi yao katika maadhimisho ya mwaka wa 50 wa uhuru wakiwa na wasi wasi lakini pia wakiwa na matumaini na fahari juu ya yaliyofikiwa nchini mwao.
Wasemayo vijana juu ya uhuru
Sibyle Munika amesema idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini, hawana mahala pakuishi na wala hakuna nafasi za ajira za kutosha kwa ajili ya vijana.Amesema anatamani kuwa na viongozi wazuri wasiokuwa mafisadi.
Joane Ochieng Onyango anayesomea taaluma ya vyombo vya habari ameeleza kuwa Kenya inasonga mbele katika tekinolojia lakini bado pana changamoto kubwa,kwa sababu "nchi yetu bado haijaendelea vizuri"
Na Samuel amejitambulisha kuwa anashughulika na mambo ya ugavishaji.Yeye ametuambia kwamba hali ya vijana wa leo ni nzuri kuliko ya wale wa miaka 50 iliyopita kwa sababu ameeleza kuwa vijana wa leo wananufaika na tekinolojia ya kisasa na zana za kileo za kupatia habari.
Ni kweli kwamba sekta ya tekinolojia ya mawasiliano na habari inastawi nchini Kenya. Wakenya ni wabunifu. Wanatayarisha programu za kompyuta kukidhi mahitaji ya wakulima, kwa ajili ya kutoa habari juu ya mambo ya afya au wanatayarisha programu za kuwezesha kufanya miamala ya fedha kwa njia ya simu, maarufu kama MPesa.
Silicon Savannah
Kiasi ya humusi moja ya pato jumla la ndani inahawilishwa kwa njia ya simu ya mkononi. Karibuni tu Kenya itakuwa kituo kikuu cha tekinolojia - Silicon Savannah ya Afrika,mithili ya Silicon Valley ya Carlifonia.
Wakati wa machafuko mnamo mwaka wa 2008 watayarishaji wa mipango ya kompyuta wa Kenya, Ushahidi, walizindua jukwaa la mawasiliano ili kutoa habari juu ya matukio ya umwagikaji damu katika sehemu za mizozo .Habari hizo ziliwasilishwa kwa watu katika ujumbe wa simu za mkononi.Wakati huo watu walihisi kwamba hawakupata habari za kutosha kutoka kwenye vyombo vya habari vya kawaida.
Mswada wa kudhibiti maudhui ya habari
Kenya ina mawanda mapana katika mandhari ya vyombo vya habari.Lakini wakati huo huo wabunge wamewasilisha kwa Rais Uhuru Kenyatta mswada wa sheria wa kuipa serikali mamlaka makubwa ya kuyadhibiti maudhui ya vyombo vya habari.
Victor Bwire ambae ni makamu mwenyekiti wa baraza huru la vyombo vya habari nchini Kenya amekasirishwa na mswada huo kwa sababu uhuru wa vyombo vya habari ni jambo lililowekwa katika katiba ya Kenya. Bwana Bwire amesema kwamba mswadaa huo una vipengele vinavyokiuka katiba.Vipengele hivyo vinaigeuza kazi ya waandishi kuwa ya kihalifu.
Hata hivyo Rais Kenyatta bado hajautia saini mswada huo.Kwa sasa ametingwa na kesi inayomkabili kwenye Mahakama Kuu ya Kimataifa ya mjini The Hague.
Kwa kuvitumia vidokezo dhidi ya ubeberu, Kenyattta anawahamasisha watu barani Afrika wasisimame dhidi ya Mahakama ya mjini The Hague ICC na anajaribu kufanya juhudi ili kesi yake iahirishwe au ikiwezekana aweze kuikwepa kabisa. Rais Kenyatta pamoja na Makamu wake William Ruto wanakabiliwa na mashtaka ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu kuhusiana na matukio ya umwagikaji damu yaliyofuatia uchaguzi wa mwaka wa wa 2007.
Mtanziko kwa nchi za magharibi
Nchi za Ulaya zinataka kesi hiyo ifanyike dhidi ya Kenyatta, lakini wakati huo huo Kenya ni mshirika muhimu wa nchi za magharibi katika harakati za kupambana na ugaidi. Kenya inashiriki katika harakati hizo nchini Somalia. Imeyapeleka majeshi yake yanayopigana kama sehemu ya majeshi ya Umoja wa Afrika.
Mwandishi: Schmidt Andrea
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Saumu Saumu