1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yailaumu Marekani

Thelma Mwadzaya7 Oktoba 2019

Kenya imeinyoshea kidole cha lawama Marekani kwa kulikataa ombi lake la kulitangaza kundi la wapiganaji la Al Shabaab kuwa la kigaidi.

https://p.dw.com/p/3QqoN
Somalia Kämpfer der Terrormiliz al-Shabaab
Picha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Hata hivyo Marekani imezipinga kauli hizo kwani inaunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa linalolitaja kundi la Alshabaab kuwa la kigaidi. Haya yamejiri kwenye kongamano la ujasusi na usalama jijini Nairobi.

Kwenye ufunguzi rasmi wa kongamano hilo la siku mbili, Spika wa bunge la Kenya  Justin Muturi aliinyoshea Marekani kidole cha lawama kwa kusita kulitaja kundi la wanamgambo wa Al Shabaab kuwa la kigaidi jambo linalowapa nafasi kuendeleza operesheni zao. Kwa mtazamo wa Kenya, hilo lilinawapa mwanya wa kuomba misaada kutoka mashirika ya kigeni yanayodai kuwa ya kutetea haki za binadamu

Balozi wa Marekani nchini Kenya ayapinga madai ya Kenya

Hata hivyo balozi wa Marekani nchini Kenya ameyapinga  madai hayo na kushikilia kuwa serikali yake haijawahi kusita kulitangaza kundi la Al Shabaab kuwa la kigaidi. Kulingana na Balozi Kyle McCarter,Marekani inaliunga mkono azimio 751 la Marekani linalolitambua kundi la Al Shabaaba kama la kigaidi.

Wakati huohuo Marekani iliweka bayana kuwa haiko tayari kuridhia pendekezo la Kenya la kutaka Somalia isitishiwe misaada yote ya kibinadamu.Viongozi hao walitoa matamshi hayo kwenye kongamano la siku mbili la usalama na masuala ya ujasusi lililoanza hii leo.

Kongamano hilo linawaleta pamoja wabunge wasiopungua 250 kujadili masuala ya usalama na wajibu wao kama viongozi na wanasiasa. Hiki ni kikao cha 15 japo kinafanyika Kenya kwa mara ya kwanza.Washirika wanatokea mataifa kadhaa kote ulimwenguni yakiwemo Marekani, Ufaransa, Ujerumani,Nigeria, Columbia, Mexico, Zambia, Argentina na Kenya iliyo mwenyeji wao. Kongamano linakamilika tarehe 8 hapo kesho.