Kenya yasaka mikopo zaidi kutoka China
16 Oktoba 2023Zaidi ya viongozi kumi na mbili kutoka Afrika, Asia na Mashariki ya Kati wamewasili mjini Beijing kwa kongamano hilo la Belt and Road Initiative (BRI) wakitanguliwa na Rais Gabriel Boric wa Chile na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán siku ya Jumapili (Oktoa 15).
Soma pia: Marekani imekua ikichukua njia mbalimbali za kukabiliana na ushawishi wa China unaozidi kuongezeka
Viongozi waliowasili siku ya Jumatatu (Oktoba 16) ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais Ranil Wickremesinghe wa Sri Lanka na mwenzake wa Jamhuri ya Kongo, Denis Sassou Nguesso, Waziri Mkuu wa Papua New Guinea James Marape na mwenzake wa Cambodia, Hun Manet.
Rais Vladimir Putin wa Urusi na wawakilishi wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan pia wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo.
Rais wa Kenya atafuta mkopo zaidi kutoka China
Katika hatua nyingine, Rais William Ruto wa Kenya ambaye pia anahudhuria kongamano hilo anatafuta mkopo wa dola bilioni moja kutoka China, licha ya kuongezeka kwa deni la umma la nchi hiyo ambalo sasa limefikia dola bilioni 70. Hii ni kulingana na takwimu za hazina ya kitaifa ya mwaka 2022/2023.
Taarifa kutoka kwa Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Hussein Mohammed, ilisema kuwa rais huyo angelitoa hotuba muhimu chini ya mada ‘Uchumi wa kidigitali kama chanzo kipya cha ukuaji' wakati wa mkutao huo wa kilele.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Rais Ruto pia angelishiriki katika mkutano wa wafadhili wa Kenya ili kusisitiza nafasi ya Kenya kama eneo la uwekezaji kwa kampuni za China .
Moja ya miradi chini ya BRI ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR
Moja ya miradi maalumu chini ya mpango huo wa BRI nchini Kenya, ni ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR inayoanzia kutoka mji wa bandari wa Mombasa hadi Bonde la Ufa kupitia mji mkuu, Nairobi.
Ujenzi wa mradi huo uligharimu dola bilioni 4.7 lakini umekabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo ucheleweshaji na kiwango cha chini cha huduma ya usafirishaji mizigo.
Kulingana na takwimu za kitaifa, Kenya imekuwa ikipambana na deni la umma linaloongezeka huku dola bilioni 6 zikiwa deni la China. Muda wa kulipa baadhi ya madeni ya nchi hiyo ni kipindi cha fedha cha 2023/2024 hali inayozidisha shinikizo zaidi kwa serikali.
Hata hivyo, haijakuwa wazi ikiwa rais Ruto na ujumbe wake wataruhusiwa kuwa na mpangilio mpya wa kulipa madeni hayo ama kuongezewa muda wa malipo ya riba.