1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yashika nafasi ya saba kwa maambukizi ya VVU duniani

1 Desemba 2023

Takwimu nchini Kenya zinaonesha nchi hiyo inashika nafasi ya saba kwenye orodha ya mataifa yenye idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI duniani, huku Rwanda na Tanzania zikitaja kufanikia kudhibiti maambukizo.

https://p.dw.com/p/4ZeqN
UKIMWI Kameruni
UKIMWI bado ni tatizo kubwa duniani.Picha: CHRISTOPHE SIMON/AFP/Getty Images

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa mataifa la maswala ya HIV, UNAIDS imebaini kuwa ulimwengu unaweza kuutokomeza Ukimwi iwapo jamii zitawezeshwa, kushirikishwa na kuungwa mkono kuongoza njia.

Tathmini hiyo imebainisha kuwa hatua zilizopigwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita zimefanikishwa na mchango wa mashirika ya kijamii.

Kwenye ujumbe Wake wa siku ya kupambana na  Ukimwi mwaka huu, Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la masuala ya Ukimwi, UNAIDS amesisitiza kuwa jamii zina nafasi muhimu katika vita dhidi ya madhila ya Ukimwi.

"Aghalabu, jamii zinatazamwa na wanaopitisha maamuzi kama vikwazo au matatizo yanayohitaji suluhu badala ya kutambuliwa na kuungwa mkono kama viongozi. Jamii sio kikwazo, ndio mwenge wa kuutokomeza Ukimwi," alisema Byanyima.

VVU UKIMWI Africa | Mwathirika Kenya na dawa za kupunguza makali
Kenya inaelezwa kuwa miongoni mw amataifa yanayokabiliwa na mzigo mkubwa wa maambukizi ya VVU.Picha: Donwilson Odhiambo/ZUMA/picture alliance

Soma pia: Kongamano la Kimataifa la UKIMWI laanza Canada

Takwimu za UKongamano la Kimataifa la UKIMWI laanza CanadaNAIDS zinaonesha kuwa mwaka 2022, watu milioni 1.3 waliambukizwa, virusi vya ukimwi, VVU, ikilinganishwa na milioni 3.2 mwaka 1995. Tathmini hiyo inaashiria kuwa wanawake na wasichana ndio wanachangia pakubwa kwa asilimia 46 ya maambukizo yote mapya kwa kipindi hicho.

Ripoti ya UNAIDS kuhusu  Ukimwi ya 2023 inaendelea kuelezea kuwa mwishoni mwa Disemba mwaka 2022, watu milioni 29.8 ambayo ni Sawa na asilimia 76 ya wote wanaoishi na virusi vya HIV wanapata dawa za kupunguza makali ya virusi hiyo, ikilinganishwa na watu milioni 7.7 mwaka 2010.

Vijana waathirika wakubwa zaidi Kenya

Kwa Kenya, serikali imeonyesha ari ya kutaka kuiongeza kasi na nguvu ya kupambana na HIV hasa baada ya maambukizi mapya kushuhudiwa kwa vijana.

Kulingana na Katibu wa kudumu katika wizara ya afya ya Kenya, Harry Kimtai, ameusisitizia umuhimu wa kuwa na juhudi za Pamoja Kati ya serikali na mashirika ya kijamii.

Soma pia:Ukimwi bado tishio

Takwimu za baraza la Taifa la kupambana na magonjwa yanayohusiana mfano Ukimwi na Kifua kikuu, NSDCC,maambukizi mapya kati ya watoto, vijana na walio katika umri wa ujana yamefikia 62 kila Wiki kwa walio na umri wa Kati ya miaka 10 hadi 19.

Baraza la NSDCC kadhalika limetangaza kuwa kaunti zinazobeba mzigo mkubwa zaidi ni Kisumu, Homabay,Siaya, Migori, Nakuru, Kakamega,Kisii, Mombasa, Kiambu na Nairobi.

Kulingana na waziri wa afya Nakhumicha Wafula, Kenya inapania kutokomeza Ukimwi  kwa watoto ifikapo 2027.

Je hofu ya ukimwi kwa vijana imepungua?

" Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Lenya itatekeleza mpango wa nguzo nne wa kuzingatia mapengo na kuiongeza kasi ya harakati za kutokomeza maambukizi ya HIV kwa watoto,” alisema waziri huyo.

Kwa Sasa, mataifa 5 ya bara la Afrika ndiyo yaliyofanikiwa kutimiza vigezo vya kupima, Kutibu na kufuatilia matumizi ya ARV za kupunguza makali ya Ukimwi yaani 95-95-95.

Mataifa hayo ni Botswana, Eswatini, Rwanda, Tanzania na Zimbabwe.