Kenya yatikiswa na wimbi jipya la maandamano ya upinzani
27 Machi 2023Matangazo
Polisi wamerusha mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji. Polisi wa kutuliza ghasia wameonekana sehemu mbalimbali mjini Nairobi.
Kinara mkongwe wa upinzani Raila Odinga ameapa kuwa hatua hiyo itaendelea licha ya marufuku ya polisi na amewataka wananchi kujitokeza barabarani kila siku ya Jumatatu na Alhamisi, licha ya maandamano ya wiki iliyopita kuzusha ghasia na vurugu.
Jana Jumapili Mkuu wa polisi nchini Kenya Inspekta Jenerali Japhet Koome alipiga marufuku maandamano mapya ya upinzani na kusema hawaruhusu maandamano yenye vurugu.
Katika maandamano ya Jumatatu iliyopita mtu mmoja aliuawa, maafisa 31 wa polisi walijeruhiwa huku watu zaidi ya 200 wakikamatwa. Hapo jana, Rais William Ruto amemtaka Odinga kuachana na azma yake ya maandamano.