1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta na makamu wake Ruto waendelea kutofautiana

Sylvia Mwehozi
22 Juni 2020

Chama tawala nchini Kenya cha Jubilee kimemtimua Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa Aden Duale, na nafasi yake itachukuliwa na mbunge Kipipiri Amos Kimunya.

https://p.dw.com/p/3e97d
Kenia Wahlen Uhuru Kenyatta und William Ruto
Picha: Reuters

Uhusiano wa siasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto ulmeendelea kusambaratika zaidi baada ya mshirika muhimu na wa karibu wa Ruto, Aden Duale kuondolewa kwenye kiti cha kiongozi wa wengi katika bunge la taifa.

Duale amekuwa kwenye wadhifa huo tangu chama cha Jubilee kipate ushindi uliozingirwa na utata katika uchaguzi mkuu mwaka 2013. Mabadiliko hayo yanajiri wakati rais Kenyatta akijitahidi kujenga urathi wake katika muhula wake wa pili na wa mwisho.

Mwenyewe amenukuliwa akisema kuwa anaondoa viongozi ambao wanaonekana kuwa vizuizi katika ajenda zake. Mkutano wa chama hicho uliodumu kwa kipindi cha dakika 25, yaelekea kuwa ulikuwa na ajenda moja tu, kumn'goa Duale. Amos Kimunya atakuwa kiongozi mpya wa wengi katika bunge la taifa.

Kenia Wahl | Protest in Nairobi | Anhänger Präsident Uhuru Kenyatta
Mfuasi wa chama cha Jubilee wakati wa kampeni za 2017Picha: Reuters/B. Ratner

Duru zinasema kuwa, kwenye mkutano wa Jumatatu, makamu wa rais William Ruto alihudhiria japo hakupewa nafasi ya kuzugumza. Alitulia na kutazama maamuzi yalipokuwa yakifanyika.

Wabunge 150 wa chama hicho walihudhuria mkutano huo, japo baadhi walituma udhuru wa kutokuhudhuria. Hatua ya makamu wa rais William Ruto ya kufungua afisi sanjari ya chama tawala kwa jina Jubilee Asili, juma lililopita huenda ilimkasirisha rais Kenyatta. Suala hilo halikujadiliwa kwenye mkutano wa Jumatatu.

Katika mkutano wa chama hicho uliofanyika majuma matatu yaliyopita Amos Kimunya alipewa nafasi ya kuwa katibu wa mikutano yote ya chama hicho. Mnadhimu mkuu wa chama hicho Benjamin Washiali na makamu wake Cecily Mbarire waliondolewa pia kwenye viti vyao.

Kenia Wahlkampf | Präsident Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta katika kampeni za Jubilee mwaka 2017Picha: Reuters/B. Ratner

Chama tawala cha Jubilee kilichoshinda uchaguzi mara mbili, kimebadilika sio haba, kwa sasa kimesaini makubaliano na vyama vya KANU, Chama cha Mashinani na Wiper, na kimejenga ushirikiano wa karibu na ODM. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa hatua hiyo ni maandalizi ya siasa za uchaguzi mkuu ujao.

Seneta Kipchumba Murkomen aliyekuwa kiongozi wa wengi katika Baraza la Seneti pamoja na makamu wa spika katika baraza hilo Kithure Kindiki, walishaondolewa kwenye viti vyao kwa kile kilichosemekana kukosa uaminifu kwa chama.

Wote walikuwa washirika wa karibu wa siasa wa Ruto. Chama kipya kinachohusishwa na Ruto cha Jubilee Asili hakijazinduliwa rasmi, lakini kinajumuisha wajumbe wote walioondolewa kwenye viti vya kamati za bunge. Makamu wa rais William Ruto na Aden Duale hawajatoa tamko lao kuhusiana na matukio hayo.

Na Shisia Wasilwa-Nairobi