Kesi ya magaidi wa NSU
6 Mei 2013Tuanzie lakini Munich ambako kesi iliyokuwa ikisuburiwa kwa hamu dhidi ya watuhumiwa wa siasa kali ya mrengo wa kulia imeanza hii leo.Gazeti la "Neue Presse" linaandika:
Kesi dhidi ya wafuasi wa vuguvugu la chini kwa chini la wazalendo wa kijamaa-NSU inaizonga jamii na idara za upelelezi,kwa masuala tete:Imekwendaje hata magaidi wakaweza kuuwa miaka nenda miaka rudi nchini Ujerumani?Kwanini waendesha mashtaka waliwatuhumu kwanza baadhi ya wahanga kuwa wanachama wa makundi ya wahalifu?Mahakama inakabiliwa na kitendawili kigumu hasa kwasababu mtuhumiwa mkuu Beate Tschäpe angali bado ananyamaza.Alikuwa msaidizi au mwasisi?Kusema kweli haiingii akilini kwamba alikuwa shahidi tuu wa kundi hilo la wauwaji-lakini jee kuna ushahidi ?
Mhariri wa gazeti la "Donaukurier" anamulika jinsi vyombo vya habari vinavyoishughulikia kesi hii na kuandika:
Si sana kumuona jaji akifuatiliziwa na vyombo vya habari kwa wiki kadhaa-na ikiwa hivyo basi mara nyingi hiyo hutoa ishara mbaya.Hata kumhusu Manfred Götzl hali ndio hiyo hiyo.Mengi yameandikwa kumhusu jaji huyo wa mahakama ya mjini Munich alieifungua hii leo kesi dhidi ya watuhumiwa wa kundi la NSU.Kwa masilahi yawahanga kumi na familia zao na zaidi kuliko yote kwa maslahi ya hadhi ya mfumo wa sheria wa Ujerumani, kilichosalia ni kutaraji kwamba jaji Götzl anastahiki jukumu alilotwikwa.
Kitisho cha kuzidi makali mzozo wa Mashariki ya kati
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na kitisho cha kuripuka zahma katika eneo la mashariki ya kati baada ya Israel kuihujumu kwa mara nyengine tena Syria.Gazeti la "Nordbayerischer Kurier" linaandika:
Mjini Jerusalem watu wanaamini serikali ya Assad imedhoofika haina tena nguvu ya kujibisha mashambulio.Lakini makombora kwa bahati mbaya hayajakosekana katika eneo hilo.Nchi zenye nguvu na ambazo zinaweza kuzishawishi pande zinazohasimiana zimlaani shetani,zimekaa kimya.Urusi inampatia silaha Assad na Marekani kwa sasa haijajitokeza na juhudi zozote za kidiplomasia.Damascus imeligeukia baraza la usalama la umoja wa mataifa lakini katika taasisi hiyo muhimu ya jumuia ya kimataifa madola yenye nguvu yanashindana.Kwa hivyo ulimwengu uko ukingoni mwa balaa.Walimwegu hawana la kufanya,wameduwaa na kujionea jinsi balaa linavyozagaa.
FDP wapania kuzusha majabu September mwaka huu
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mkutano mkuu wa chama cha kiliberali cha FDP uliomalizika jana mjini Nürnberg.Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika:
Mara ngapi watu wamekuwa wakiashiria FDP kimekwisha?Wachunguzi wa maoni ya umma wanakitaja kuwa chama cha mgawanyiko hata wasanii wa vichekesho wanakiita chama hicho cha kiliberali "sarakasi".Mkutano mkuu wa Nürnberg lakini umedhihirisha FDP kipo.Na ikiwa wapinzani wake wataendelea kupigania kodi za mapato ziongezwe,basi si hasha FDP wakaendelea kuwepo madarakani.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu