1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya mauaji inayomkabili Musharraf yaahirishwa

6 Agosti 2013

Rais wa zamani wa Pakistan Pervez Musharraf amekosa kufika mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto kwa kile polisi imesema ni sababu za kiusalama.

https://p.dw.com/p/19KKN
Picha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Musharraf aliyeliongoza taifa la Pakistan kati ya mwaka 1999 hadi 2008 alikuwa ametakiwa kufika mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili ya kupanga njama za uhalifu na mauaji ya Bhutto mnamo mwezi Desemba mwaka 2007.

Lakini polisi na wakili wake wameiambia mahakama ya Rawalpindi mji ambao Bhutto aliuawa kuwa si salama kumfikisha Musharraf mahakamani kutokana  na vitisho vya mauaji dhidi yake.

Musharraf ashindwa kufika mahakamani

Jaji Chaudry Habibur Rehman ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe 20 mwezi huu na kuagiza kiongozi huyo wa zamani kufikishwa siku hiyo.Hata hivyo kumekuwa na fununu kuwa kuna mipango ya chini kwa chini itakayomuwezesha Musharraf kuondoka nchini humo bila kuhukumiwa na kuyumbisha jeshi la nchi hiyo.

Musharraf ambaye amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu mwezi April mwaka huu alifikishwa mahakamani binafsi tarehe 30 mwezi uliopita.

Rais wa zamani wa Pakistan Pervez Musharraf
Rais wa zamani wa Pakistan Pervez MusharrafPicha: SAEED KHAN/AFP/Getty Images

Wakati huo huo wanajeshi watano wa India wameuawa kwenye shambulio dhidi ya kituo cha kijeshi katika eneo la mpakani linalozozaniwa na Pakistan la Kashmir huku nchi hizo mbili zikijiandaa kufufua mazungumzo ya amani.

Haijabainika wazi ni nani aliyehusika na mashambulio hayo.Jeshi la Pakistan limekanusha kuhusika na kuyataja madai ya kuhusika kuwa kuwa yasiyo na msingi wowote.

Mazungumzo yatiliwa shaka

India imetangaza kujiondoa kutoka mazungumzo hayo ya amani na Pakistan yaliyopangiwa kuanza.Mauaji hayo yamezua ghadhabu katika bunge la India huku wabunge wakitaka maelezo ya kina kutoka kwa serikali.Waziri wa ulinzi A.K Antony anatarajiwa kutoa taarifa bungeni baadaye leo.

Mwanajeshi wa India katika eneo linalozozaniwa la Kashmir
Mwanajeshi wa India katika eneo linalozozaniwa la KashmirPicha: Roufb Bhata/AFP/Getty Images

Mwezi uliopita,serikali mpya ya Pakistan inayoongozwa na waziri mkuu Nawaz Sharrif ilipendekeza tarehe za kuanza kwa mazungumzo na India ilikuwa inajitayarisha kutoa tamko kuhusu pendekezo hilo.   

Amani ya kudumu kati ya Pakistan na India ambazo zimepagana vita mara tatu tangu nchi zote mbili kujinyakulia uhuru mwaka 1947 imeonekana kuwa vigumu kuafikia.

Wachambuzi wengi wanahisi ni muhimu zaidi kwa nchi hizo kupunguza uhasama kufuatia kuondoka kwa majeshi ya kigeni katika taifa jirani la Afghanistan ifikapo mwaka ujao na kuzua hofu ya kuongezeka kwa mzozo nchini humo.

Kabla ya mauaji hayo kumekuwa na uwezekano wa kufanyika kwa mkutano kati ya waziri mkuu wa Pakistan Shariff ambaye wakati wa kampeini za uchaguzi aliahidi kuboresha uhusiano na India  na mwenzake wa India Manmohan Singh pembezoni mwa  mkutano mkuu wa Umoja wa mataifa mwezi ujao mjini Newyork.

  India inadai kuwa Pakistan inawapa silaha na kuwahifadhi wanamgambo wa Kashimiri.Pakistan imekanusha kuwapa silaha wanamgambo hao na kusema inaunga tu mkono watu wa Kashmir.

Kumekuwa na mashambulio makali dhidi ya vikosi vya usalama vya India mjini Kashmir  mwaka huu.Kulingana na maafisa wa India,kiasi ya wanamgambo 25 wameuawa na wanajeshi wa India katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Ssessanga Iddi