1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya "Nyaraka za Panama" yaanza baada ya miaka minane

9 Aprili 2024

Miaka minane baada ya kuibuliwa kwa kashfa kubwa kabisa ya kifedha ya kimataifa iliyopewa jina la "Nyaraka za Panama", kesi ya kwanza dhidi ya watuhumiwa 27 imeanza nchini Panama.

https://p.dw.com/p/4eYxT
Jurgen Rolf Dieter Mossack
Jurgen Rolf Dieter Mossack, mmoja wa watuhumiwa wa kesi ya "Nyaraka za Panama."Picha: Aris Martinez/REUTERS

Nyaraka hizo zilisambazwa majira ya machipuko ya mwaka 2016 kutokana na data zilizovujishwa za kampuni ya sheria ya Mossack Fonseca nchini Panama, ambazo zilichambuliwa na timu maalum ya waandishi wa habari duniani kote.

Waandishi hao waligunduwa kwamba wanasiasa, wanariadha na watu wengine mashuhuri ulimwenguni walikuwa wanamiliki mali nyingi nje ya mataifa yao.

Soma zaidi: Wachezaji watajwa katika "Nyaraka za Panama"

Mmiliki mwenza wa kampuni hiyo, mwanasheria aliyezaliwa Ujerumani, Jürgen Mossack, alipandishwa kizimbani mjini Panama City siku ya Jumatatu (Aprili 8), kwenye siku ya kwanza ya kesi hiyo iliyokuwa ikitangazwa moja kwa moja mtandaoni.

Watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa kutakatisha fedha kupitia kuanzisha kampuni 215,000 hewa ili kukwepa kodi.

Mossack, mwenye umri wa miaka 76, alikanusha kuhusika na mashitaka hayo, na kesi hiyo sasa itasomwa tena wiki tatu zijazo.