1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha msichana Mahsa chazusha maandamano makubwa Iran

20 Septemba 2022

Maandamano yazuka nchi nzima ya Iran na watu wasopungua 5 wameuwawa

https://p.dw.com/p/4H62X
Protest im Iran
Picha: UCG

((Nchini Iran maandamano yamezuka kufuatia kifo cha msichana wa miaka 22 kilichotokea akiwa mikononi mwa polisi. Msichana huyo alikamatwa kwa kosa la kutojifunika vizuri vazi la hijabu kama ilivyo sheria nchini Iran.Watu kadhaa wameuwawa kufuatia vurugu za maandamano hayo.

Maandamano katika mji mkuu Tehran yalianza jana Jumatatu jioni na katika nchi nzima ya jamhuri ya kiislamu ya Iran,watu waliojawa na ghadhabu walimiminika mitaani baada ya kifo cha  Mahsa Amin msichana aliyekuwa na umri wa miaka 22 aliyekamatwa na wale wanaoitwa polisi wa maadili nchini Iran  kwa tuhuma za kutozingatia sheria ya uvaaji vazi la hijabu.

Iran | Proteste nach Tod von Mahsa Amini
Picha: AP/dpa/picture alliance

Na hayo ni kwa mujibu wa zipoti za vyombo vya habari.Inaelezwa kwamba Mahsa alikamatwa Septemba 13 nje ya kituo cha usafiri wa treni mjini Tehran akitokea kwao Saqez, mji ulioko kwenye jimbo la wakurdi huko Iran,alikwenda Tehran kwa ajili ya kutembelea jamaa zake.

Lakini hivi karibuni ikaelezwa kwamba alifia mikononi mwa polisi baada ya kupigwa vibaya akiwa kwenye karandika ya polisi hao wa maadili waliomata.Imeelezwa kwamba alipelekwa kituo cha polisi na kushikiliwa kwa muda wa saa moja ambako huko alipewa kile kilichotajwa kuwa ni kuelimishwa tena.

Ingawa pia kwa upande mwingine inaelezwa wakati alipokuwa akisubiri  nje ya kituo cha polisi cha Vozara ambako kuna jela ya kuwashikilia wanawake waliokamatwa na polisi hao wa maadili, ilikuja gari la wagonjwa na kumchukua msichana huyo wa kikurdi na kumpeleka katika hospili ya Kasra,Kakaake aliyezungumza na vyombo vya habari anasema alikuwa ameshapoteza fahamu.Alifariki tarehe 16,ni wiki iliyopita.

Mamlaka zimesema kifo chake kimetokana na mshtuko wa moyo.

Iran Sanandaj Protest gegen Tod von Mahsa Amin
Picha: NNSRoj

Kifo cha msichana huyo kimeibuwa hasira kubwa miongoni mwa wananchi wa Iran na maandamano yameshuhudiwa nchi nzima na ripoti za hadi wakati huu zinaeleza kwamba watu kiasi ya watano wameuwawa katika maandamano hayo kwenye mkoa wa kikurdi baada ya vikosi vya usalama kuwafyetulia risasi waaandamanaji kutaka kuwatawanya.

Mazingira ya kifo cha msichana Mahsa ambaye pia anafahamika kwa jina maarufu Zhia bado ni suala la mjadala unaozusha malumbano nchini Iran. Kote nchini Iran sauti zimeongezeka za kulaani tukio la kifo cha msichana huyo na kwa mara nyingine kimeliibua suala la sheria ya kuwalazimisha wanawake kuvaa hijabu na athari zake.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW