Uchambuzi: Kifo cha Navalny pigo kwa upinzani nchini Urusi
19 Februari 2024Wakosoaji wa kisiasa wa ikulu ya Kremlin, waliogeuka serikali na waandishi wa habari za upelelezi wameuawa au kushambuliwa kwa njia mbalimbali nchini Urusi.
Miaka minne iliyopita, Navalny aliulizwa na mtayarishaji mmoja wa filamu kile anachoweza kuwaambia raia wa Urusi iwapo angeuawa kwa kumpinga rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin. Kiongozi huyo wa upinzani alijibu kwa kusema hairuhusiwi kukata tamaa na kwamba kama serikali itaamua kumuua, ina maana kwamba upinzani una nguvu kubwa na unahitaji kutumia nguvu hiyo.
Siku ya Ijumaa, idara ya magereza ya Urusi ilitangaza kuwa Navalny amefariki dunia katika gereza alikokuwa anatumikia kifungo cha miaka 19 kwa hatia za itikadi kali.
Kifo hicho kimeibua shutuma kote duniani kwamba ameuawa, ingawa si pekee kufariki kwenye mazingira ya kutatanisha. Viongozi wengi wa upinzani wa Urusi aidha wamefariki, wamekimbilia uhamishoni nje ya nchi ama wamefungwa magerezani nchini humo.
Makundi ya upinzani yaliyosalia na viongozi wakuu wa kisiasa wana maono tofauti kuhusu jinsi Urusi inapaswa kuwa na nani anayepaswa kuiongoza. Kwa mfano, hakuna hata mgombea mmoja anayepinga vita vya Urusi dhidi ya Ukraine anayeshiriki katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwezi ujao kutoa ushindani kwa Putin anayegombea kubaki uongozi kwa muhula wa sita.
Soma pia:Urusi bado haijathibitisha sababu za kifo cha Navalny
Baada ya kifo cha Navalny, wengi wanajiuliza kama huu ndio mwisho wa upinzani wa kisiasa nchini Urusi.
Mikhail Khodorkovsky, tajiri wa zamani ambaye alifungwa jela kwa miaka kumi kwa mashtaka ambayo kwa kiasi kikubwa yalionekana kuwa ya kisasi cha kisiasa kwa kupinga utawala wa Putin mwanzoni mwa miaka ya 2000, amesema kuwa Navalny alikuwa kiongozi muadilifu na mwenye kipachi cha kuwashawishi watu kuhusu mahitaji ya mabadiliko.
Khodorkovsky ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba upinzani nchini Urusi umepata pigo kubwa kutokana na kifo hicho cha Navalny.
Graeme Robertson, profesa wa sayansi ya kisiasa katika chuo kikuu cha North Carolina ambaye pia ni mwandishi wa kitabu kuhusu Putin na siasa za kisasa nchini Urusi, amesema tatizo kubwa ambalo limeukumbuka upinzani wa Urusi ni kwamba umeshindwa kujiondoa kutoka kwa makundi madogo ya kiliberali ili kuvutia uungwaji mkono kutoka kwa idadi kubwa ya watu.
Khodorkovsky, anayeishi mjini London nchini Uingereza, ni mmoja kati ya wapinzani kadhaa wa kisiasa wa Urusi wanaojaribu kuunda muungano na makundi ya mashinani yanayopinga vita kote ulimwenguni pamoja na wanasiasa wa upinzani wa Urusi walio uhamishoni.
Lakini kundi la Navalny na wakfu wa kupambana na ufisadi aliouanzisha sio sehemu ya mchakato huo.
Mwenendo wa Navalny uliwachukiza baadhi wa wapinzani
Katika mahojiano mengine kabla ya kifo cha Navalny, Khodorkovsky alisema kwamba mara kwa mara wamekuwa wakiwaambia wahusika wa wakfu huo wa Navalny kwamba itakuwa jambo zuri ikiwa wote wangekutana sio tu mbele ya kamera za televisheni lakini kuketi katika meza moja.
Huku Navalny akiwa kiongozi wa kwanza kuanzisha upinzani wa kitaifa wa Urusi, kuna vyama vingine vya upinzani ambavyo havikumpenda ama shirika lake.
Kabla ya kifo chake, kulikuwa na tofauti kali za hadharani katika mitandao ya kijamii kati ya wanachama wa kundi lake na wanasiasa wengine kuhusu jinsi wangeweza kumpinga Putin katika uchaguzi ujao wa mwezi Machi.
Soma pia:Mjane wa Navalny kukutana na mawaziri wa EU
Wakati huo huo, Putin ameendelea kuimarisha udhibiti wake madarakani, kukandamiza upinzani nchini humo, kuwafunga wakosoaji wa vita nchini Ukraine, na kufungia vyombo huru vya habari.
Kwa sasa, upinzani nchini Urusi unakabiliwa na mustakabali usio na mwanga kutokana na kumkosa mmoja wa viongozi wake mahiri.
Itakuwa vigumu sana, lakini wanasiasa wa Urusi walio uhamishoni wanasema wamejitolea kuona kwamba matumaini ya demokrasia nchini mwao yanatimia na sio kuangamia pamoja na kifo cha Navalny.