Kifo cha Nkurunziza: Viongozi watuma salamu za rambirambi
10 Juni 2020Rais wa zamani Domitien Ndayizeye amesema licha ya kuwa bado ni mapema wanatambua kuwa kulingana na katiba
atakaye iongoza nchi kimpito ni spika wa bunge.
Kifo cha rais Pierre Nkurunziza kimezusha hali ya taharuki kwa raia wengi. Shughuli zimeonekana kudorora,
huku redio na televisheni ya taifa ikibadili ratiba na kucheza nyimbo peke za dini za maombolezi.
Maafisa wakuu wa taasisi mbali mbali ikiwa ni pamoja na spika wa bunge, mkuu wa seneti, makamu
wa rais, Mawaziri wa serikali, Msuluhishi wa kitaifa, baadhi ya wanasiasa, na hata raia wa kawaida wametowa
salaam za rambi rambi kwa familia yake rais Nkurunziza na chama chake Cndd Fdd.
Pia wanabalozi wa nchi za Kenya, Misri, Nigeria, Cote d, ivoire, Uturuki, China, na urusi tayari wamesaini kwenye kitabu cha maombole
kilozinduliwa kwenye ikulu ya rais.
Risala za maombolezi zimetolewa pia na marais wa zamani. Domitien Ndayizeye aliyefanya naye kazi Nkurunziza kama waziri wake wa dola anaye
husika na utawala bora, amesema kuna umuhimu serikali kubaini kitakacho fuatia. Hata hivyo amesema katiba iko wazi ambapo atakaye
ongoza kimpito ni spika wa bunge.
Chama cha hayati Nkurunziza cha Cndd Fdd bado hakijatoa taarifa yoyote, mbali na rais mteule Evariste Nsayishimiye aliyeshinda kwenye uchaguzi
ulofanyika Mei 20 kutowa salam za rambi rambi na kubainisha kuwa ataendelaza sera yake rais Nkurunziza.
Taarifa ya kifo cha rais Pierre Nkurunziza ilitangazwa na serikali hapo jana na kueleza kuwa kifo chake kimesababishwa na
mshituko wa moyo.
Licha ya kazi kuendelea kufanyika, serikali ilitangaza Msiba wa kitaifa wa siku 7 ambapo bendera zinapandishwa nusu mlingoti.
Rais Pierre Nkurunziza alifariki Jumatatu wiki hii baada ya kuiongoza Burundi kwa muda wa miaka 15.
Amida ISSA, DW -BUJUMBURA