Kila Mmoja ni Tofauti - Heshima kwa Makundi ya Wachache
6 Agosti 2013Mara nyingi makundi ya watu wachache hutengwa na jamii. Wanabaguliwa kwa sababu hawako sawa na watu wengi wanaowazunguka. Mfululizo wa vipindi hivi unaonyesha kuwa watu wenye kasoro za kimaumbile, fikra au tabia tofauti, wana haki ya kuchukuliwa kama binaadamu wengine wowote wale. Vipindi hivi pia vinaonyesha idadi ya makundi ya wachache yanayolazimika kupigania kukubaliwa katika jamii.
Mmoja wa wahusika wakuu katika mchezo huu ni John, muimbaji mwenye kipaji na mwandishi wa nyimbo anayeishi nchini Zambia. John ameandika wimbo wa mapenzi ambao umemfanya kuwa maarufu sana kote nchini. Mwanamuziki huyo chipukizi anapendwa sana na mashabiki wake. Hata hivyo hisia hizi za kukubalika miongoni mwa jamii ni jambo geni kwake. John ana ulemavu wa ngozi na alikulia katika kijiji ambako alitengwa na wengi katika jamii. Licha ya ufanisi wa kustaajabisha wa John, watu wengine wenye ulemavu wa ngozi nchini Zambia bado wanakabiliwa na ubaguzi na ukatili.
Junior, kijana ambaye ni shoga, alikabiliwa na unyanyapaa kama huo. Alikuwa akiishi Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lakini kwa kuwa mara kwa mara alihofia maisha yake, akahamia nchini Afrika Kusini. Hata huko Afrika Kusini, inayosemekana kuwa nchi inayowakubali na kuwajali mashoga barani kote Afrika, Junior bado havumiliwi kila mahali.
Wasikilizaji wa mchezo huu pia wanakutana na Mnigeria Lois, mlemavu anayetembea kwa kiti cha magurudumu. Ingawa anakabiliwa na changamoto ngumu katika maisha yake ya kila siku, Lois bado anapata nguvu za kuwatia moyo watu wengine wenye ulemavu kupigania haki zao.
Katika vipindi kumi vya mchezo huu, wanachama wa makundi tofauti ya wachache barani Afrika na hata Waafrika wanaoishi nje ya bara hilo, wanatoa maoni yao na kuwatia moyo wasikilizaji kuwaheshimu.
Vipindi vya Noa Bongo Jenga Maisha Yako hutayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika lugha sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.