Kilio cha jamii za kiasili
Kila mwakaAgosti 9, Umoja wa Mataifa huhamasisha ulinzi wa jamii za kiasili. Kuadhimisha siku hii, DW inaangazia ni mazingira gani yanayowakabili watu hawa katika zama hizi?
Matajiri wa tamaduni, maskini wa maisha
Kuna watu wa sili milioni 370 walioenea kote ulimwenguni, katika nchi 90, na idadi kubwa, kama asilimia 70 wanaishi Asia. Ni watu kutoka jamii zaidi ya 5,000 tofauti na wanaongea lugha zaidi ya 4,000. Ijapokuwa wanaunda asilimia tano ya idadi ya watu ulimwenguni, asilimia 15 ya watu masikini kabisa duniani inaundwa na jamii hizi.
Ubaguzi wa kitamaduni na ukandamizaji
Katika nchi nyingi, watu wa kiasili wametengwa kwa kiasi kikubwa kuanzia kisiasa, kiuchumi na kitamaduni na wanajitahidi kudumisha utambulisho wao wa kitamaduni. Mara nyingi hutendewa kama raia wa daraja la pili na hukutana na visa vya kubaguliwa na kukandamizwa.
Kufukuzwa
Kubwa ambalo huchochea mizozo ni ardhi zao za asili, ambazo wameishi kwa vizazi, wakati mwingine kwa makumi ya maelfu ya miaka. Licha ya kuwa na haki za umiliki wa ardhi ambazo zinatambuliwa chini ya sheria za kimataifa, mara nyingi hufukuzwa kutoka katika ardhi zao, ambazo huuza, kukodisha au kunyang'anywa tu na serikali ama kampuni binafsi.
Kupoteza uoto wa asili
Ardhi ya mababu ya watu wa asili inakaliwa na zaidi ya asilimia 80 ya viumbe hai vya sayari yetu na ina utajiri wa maliasili, kama vile mafuta, gesi, mbao na madini. Watu asilia wanayo maarifa muhimu ya jinsi ya kusimamia maliasili kwa vitendo na huwa kama walinzi wa ardhi kwa kizazi kijacho. Lakini watu wengi wa kiasili wameondolewa katika ardhi yao.
Mpiga picha aliyeangazia kilio cha watu wa kiasili
Mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya upigaji picha za Sony World aliangazia kilio cha watu wa kiasili na wa jadi na ardhi ambayo wananyang'anywa. Picha hii iliyopigwa na mpiga picha wa Uruguay Pablo Albarenga inaonyesha kijana wa kiasili kutoka Jimbo la Achuar huko Ecuador ambaye anayejihusisha na kukomesha utegemezi wa Achuar kwenye petroli kwa kufunga paneli za jua kwenye boti zao.
Watu wa Amazoni waapa kulinda ardhi yao
Tangu Bolsonaro, aliyewafananisha watu asilia na wanyama, alipoingia madarakani nchini Brazil kumekuwa na ongezeko la uvamizi wa wachimbaji na wakata mbao kwenye ardhi ya watu wa asili na viongozi saba wa jamii za asili wameuawa katika mizozo ya ardhi. Kumekuwa na ongezeko la moto na ukataji miti. Licha ya vitisho, watu wa asili wa msimu wa Amazonia wameapa kulinda ardhi yao na namna wanavyoishi.
Wanawake wa asili wa Colombia wapinga dhuluma za kijinsia
Huko Colombia, wanawake wa kiasili mara nyingi huwa wahanga wa dhuluma za kijinsia. Mnamo Juni, askari saba kutoka genge la wanajeshi la Colombia walimbaka msichana mdogo wa asili. Na kwa bahati mbaya, halikuwa tukio la pekee. Tangu wakati huo, wanawake wa kiasili wameanza kufanya maandamano hadharani, wakiwa na mabango, wakiimba na kucheza.
Watetezi wa haki za binaadamu wa jamii za kiasili washambuliwa
Si salama wakati wote kuzipigania haki zao hadharani. Mwaka jana kulishuhudiwa idadi kubwa ya watetezi wa haki za binadamu waliouawa nchini Colombia: Jumla yao walikuwa 107. Ulimwenguni kote, watetezi wa haki za binadamu wa jamii za asili ambao walizungumza dhidi ya sera za kibaguzi walikabiliwa na vitisho na maonyo.
Ulinzi unatakiwa
Kupunguzwa kwa rasilimali na mila zilizo muhimu kwa maisha yao, watu wengi wa kiasili sasa wanakabiliwa na umaskini mkubwa, magonjwa na vurugu - na wakati mwingine, kutoweka. Huku mabadiliko ya hali ya hewa yakizidi kuongezeka, watu hawa wa asili wanakabiliwa na kitisho kikubwa zaidi na Umoja wa mataifa unasema ni muhimu kuyalinda maisha yao.