Kim Jong Un asimamia urushaji wa kombora jipya
15 Februari 2024Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, jana Jumatano alisimamia jaribio la ufyatuaji wa kombora jipya kutoka ardhini hadi baharini na kutembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza silaha.
Jeshi la Korea Kusini lilisema kuwa Korea Kaskazini ilirusha makombora mengi kutoka pwani yake ya mashariki jana Jumatano. Shirika la habari la Korea Kaskazini la KCNA limelitaja kombora hilo jipya kuwa ni Padasuri-6, na liliruka juu ya bahari na kufikia eneo lililokusudiwa.
Aidha, shirika la habari la KCNA limemnukuu Kim aliyesema kwamba Korea Kusini inakiuka mamlaka ya Kaskazini na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu mipaka ya baharini kati ya nchi hizo mbili. Kim ametoa amri ya kuimarisha utayari wa kijeshi katika eneo la baharini, kaskazini mwa Kisiwa cha Yeonpyeong na magharibi mwa rasi ya Korea.