1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Hidaya chaharibu miundombinu Tanzania

6 Mei 2024

Mawasiliano kati ya mkoa wa Dar es Salaam na mikoa iliyopo Kusini mwa Tanzania ya Lindi, Mtwara na Ruvuma yamekatika baada ya miundombinu ya barabara kuharibika.

https://p.dw.com/p/4fXql
Tanzania | Mafuriko kutokana na kimbunga Hidaya
Mvua hizo zinatajwa kuharibu, zaidi ya madaraja manne yalipo kwenye barabara kuu ya Mtwara – Dares Salaam.Picha: Communications department Ministry of Public Works Tanzania

Miundombinu iliyoharibiwa ni pamoja na madaraja kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zilizoambatana na Kimbunga Hidaya, nchini Tanzania. 

Mvua hizo zinatajwa kuharibu, zaidi ya madaraja manne yalipo kwenye barabara kuu ya Mtwara – Dares Salaam, katika maeneo ya wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, hivyo kukata mawasiliano katika mikoa ya Kusini, na kupelekea adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa mikoa hii, ambao wengi hutegemea kufanya shughuli mbalimbali katika mkoa wa Dar es saalam.

Wananchi waliokuwa wanasafiri kutoka mkoa wa Dar es Salaam kuja katika mikoa hii ya kusini, kutoka katika mikoa hii kwenda Dar es Salaam wamekwama, katika eneo la Somanga Mtama, huku kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kufanikisha malengo ya safari zao.

Safari ndefu kufika Dar es Salaam

Kutokana na changamoto hiyo baadhi ya abiria wanalazimika kusafiri kuelea Dar es Salaam kupitia Barabara ya mkoa wa Ruvuma, Iringa, na Morogoro ambako usafiri kwa zaidi ya kilometa 2,000 na kulazimika kulipa nauli ya shilingi 120,000, tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambako walikuwa wanasafiri wastani wa umbali wa kilometa 700 na kulipa nauli ya  shilingi 38,000.

Soma pia: Tanzania yasema kimbunga Hidaya sio kitisho tena baada ya kupungua kasi,japo umma watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari.

Tansania | Überschwemmungen nach Zyklon Hidaya
Sehemu ya barabara iliyoharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Hidaya eneo la Somawanga, Lindi nchini Tanzania.Picha: Communications department Ministry of Public Works Tanzania

Hata hivyo, Serikali imewataka wamiliki wa magari ya abiria kuwarudisha abiria wa kwenye mabasi yao mahali walikowatoa kwa kuwa hakuna uwezekeano wa kuendelea na safari na eneo hilo kutokuwa salama kutokana na mvua kuendelea kunyesha.

Lakini pia kuwaepusha wananchi dhidi ya hatari ya kutokea kwa mlipuko wa magonjwa mbalimbali kutokana na kuwepo kwa mrundikano wa watu katika eneo hilo ambalo halina mbiundombinu muhimu kama ya choo.

Serikali yatangaza siku tatu za matengenezo ya barabara Somanga

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, amefika katika eneo la Somanga, wilayani Kilwa mkoani Lindi ili kujionea hali ilivyo  na kutangaza siku tatu za matengezo ya barabara hiyo.

Serikali yawaomba wahanga wa mafuriko kuwa wavumilivu

Mbali na maafa hayo kupelekea athari za miundombinu,  Kamanda wa Zima moto na uokoaji mkoani Lindi Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabije  amesema, mvua hizo zimesababisha vifo vya watu wawili, na wengine zaidi ya 80 wameokolewa katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Ambapo 49 kati yao walikuwa mashambani na wengine 31 majumbani.