1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Kiongozi mpya Syria aahidi kuheshimu mamlaka ya Lebanon

22 Desemba 2024

Wiki mbili baada ya kuchukua madaraka, kiongozi mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, ameimarisha mawasiliano ya kikanda, akiahidi katika mkutano wa Jumapili kutokuhusika "kwa njia hasi" nchini Lebanon.

https://p.dw.com/p/4oULV
Syria Damascus 2024 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Fidan akutana na Kiongozi mpya wa Syria Al-Sharaa
Kiongozi mpya wa Syria Ahmed Al-Sharaa (kulia) akiwa katika mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan mjini Damascus, Desemba 22, 2024.Picha: Turkish Foreign Ministry/DIA Images/ABACA/picture alliance

Sharaa pia alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, baada ya waasi wanaoungwa mkono na Ankara kulisaidia kundi lake la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), ambalo liliteka mji wa Damascus mnamo Desemba 8 na kumuondoa mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad.

Uturuki imeendeleza uhusiano wa karibu na viongozi wapya wa Syria, na mkuu wa intelijensia wa Ankara, Ibrahim Kalin, aliitembelea Damascus siku nne tu baada ya kuanguka kwa Assad.

Dola kubwa la kikanda Saudi Arabia pia imo katika mawasiliano ya moja kwa moja na mamlaka mpya za Syria, baada ya kuunga mkono upinzani dhidi ya Assad kwa miaka mingi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, na itatuma ujumbe hivi karibuni, kulingana na balozi wa Syria mjini Riyadh.

Syria Damascus 2024 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Fidan akutana na Kiongozi mpya wa Syria Al-Sharaa
Kiongozi wa utawala mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, akisubiri kuwasili kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, kabla ya mkutano wao mjini Damascus, Syria, tarehe 22 Desemba 2024.Picha: Arda Kucukkaya/Anadolu/picture alliance

Syria kutojihusisha kwa "njia hasi" Lebanon

Wakati wa mkutano wake na viongozi wa Druze wa Lebanon, Walid na Taymur Jumblatt, Sharaa alisema Syria haitahusika tena "kwa njia hasi nchini Lebanon hata kidogo."

Aliongeza kuwa Damascus "inaheshimu mamlaka ya Lebanon, umoja wa ardhi yake, uhuru wa maamuzi yake na uthabiti wa usalama wake." 

Soma pia: Watawala wapya Syria wateua waziri wao wa mambo ya nje

Syria "itakuwa umbali sawa na kila mmoja" nchini Lebanon, Sharaa aliongeza, akikiri kuwa Syria imekuwa "chanzo cha hofu na wasiwasi" kwa nchi hiyo. 

Walid Jumblatt, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mkosoaji mkali wa Assad na baba yake Hafez aliyekuwa mtawala wa Syria kabla yake, aliwasili Damascus Jumapili akiwa ameongoza ujumbe wa wabunge kutoka kundi lake la bunge na viongozi wa kidini wa Druze.

Dini ya wachache ya Druze iko katika Lebanon, Syria, na Israeli.

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

Alikutana na Sharaa -- anayejulikana pia kama Abu Mohammed al-Jolani -- katika ikulu ya rais, ambapo kiongozi mpya wa Syria alivaa suti na tai badala ya shati la kijeshi la kijani alilovaa siku chache zilizopita. 

Walid Jumblatt anazishutumu mamlaka za zamani za Syria kwa kumuua baba yake mwaka 1977 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon.

Jeshi la Syria liliingia Lebanon mwaka 1976, na kuondoka mwaka 2005 baada ya shinikizo kubwa kufuatia mauaji ya waziri mkuu wa zamani Rafic Hariri, mauaji yaliyohusishwa na Damascus na mshirika wake, kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon. 

Assad alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Alawite ya Uislamu wa Shia na alijitambulisha kama mlinzi wa wachache wa kidini na kikabila wa nchi hiyo.

Soma pia: HTS kujivunja na kujiunga na jeshi la Syria

Kuchukuliwa kwa madaraka na Waislamu wa Sunni wa HTS -- waliotajwa kama shirika la kigaidi na serikali nyingi ikiwemo Marekani -- kumewatia wasiwasi wengi, ingawa kundi hilo limejaribu hivi karibuni kupunguza kauli zake kali.

Mataifa yapishana kuanzisha ushirikiano na HTS

Pamoja na wasiwasi kuhusu mustakabali wa Syria, madola makubwa zikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya yameimarisha mawasiliano na viongozi wapya wa nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na vita, yakiwataka kuhakikisha ulinzi wa wanawake na wachache.

Viongozi wa kigeni pia wameelezea umuhimu wa kupambana na "ugaidi na misimamo mikali." 

Syria, Damascus | Mkutano kati ya Tobias Tunkel na Ahmed Al-Sharaa
Ahmed Al-Sharaa pia alikutano wa Mjumbe wa Serikali y aUjerumani kwa Kanda ya Mashariki ya Kati, Tobias Tunkel mjini Damascus, baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad.Picha: SANA/AFP

Kiongozi mkuu wa Iran -- ambaye alikuwa msaidizi muhimu wa utawala wa Assad kabla ya kuanguka mikononi mwa waasi -- Jumapili alitabiri "kuibuka kwa kundi lenye nguvu na heshima" ambalo litapambana dhidi "ukosefu wa usalama" nchini Syria.

Ayatollah Ali Khamenei alisema vijana wa Syria watasimama "kwa nguvu dhidi ya wale waliobuni hali hii ya kutokuwa na usalama na wale waliotekeleza, na kwa mapenzi ya Mungu, watawashinda." 

Soma pia: Mjumbe wa UN Syria ataka vikwazo viondolewe baada ya Assad

Assad kwa muda mrefu alikuwa na jukumu la kimkakati katika "mhimili wa upinzani" wa Iran, muungano usio rasmi wa makundi ya uwakala wa kikanda, hasa katika kuwezesha usambazaji wa silaha kwa Hezbollah nchini Lebanon jirani.

Mhimili huo umepata pigo kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, huku Israel ikiangamiza uongozi wa Hezbollah nchini Lebanon na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo, Khamenei alikanusha kwamba vikundi hivi vya silaha vilikuwa mawakala, akiongeza kuwa: "Iwapo siku moja tutataka kuchukua hatua, hatuhitaji kikosi cha wakala."