1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Kiongozi na wafuasi 20 wa genge la uhalifu Haiti wauawa

16 Oktoba 2024

Kiongozi wa moja ya magenge yenye nguvu zaidi nchini Haiti amejeruhiwa katika tukio la ufyetulianaji risasi na polisi ya Haiti na Kenya katika uvamizi wa kwanza mkubwa kwenye eneo linalodhibitiwa na magenge.

https://p.dw.com/p/4lqTI
Polisi washika doria katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-prince baada ya kuwatawanya waandamanaji mnamo Agosti 19, 2024
Polisi washika doria katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-prince Picha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Katika taarifa, polisi ya taifa nchini Haiti imesema kamanda wa pili wa genge la Kraze Baryè, anayejulikana kama "Deshommes," alipigwa risasi huko Torcelle, eneo linalodhibitiwa na genge hilo kusini mashariki mwa mji mkuu Port-au-Prince.

Wanachama 20 wa genge la Kraze Baryè nchini Haiti wauawa 

Maafisa wa polisi wamesema kuwa wanachama wengine 20 wa genge hilo waliuawa wakati wa operesheni zilizofanywa siku ya Jumamosi na Jumatatu, na kuongeza kuwa walinasa bunduki, risasi, simu pamoja na vifaa vingine.

Polisi imesema msako huo utaendelea hadi genge hilo na kiongozi wake mkuu Vitel'Homme Innocent, litakapodhibitiwa.

Katika taarifa, polisi ya Kenya inayoongoza ujumbe huo wa Haiti, imetoa wito kwa Innocent kukoma kufanya ukatili dhidi ya raia wa Haiti wasiokuwa na hatia.

Kiongozi wa muungano wa magenge ya silaha Jimmy "Barbecue" Cherizier, afyetua risasi hewani baada ya kuhutubia waandishi wa habari mjini Port-au-Prince, haiti mnamo Machi 11,2024
Kiongozi wa muungano wa magenge ya silaha Jimmy "Barbecue" Cherizier, afyetua risasi hewani mjini Port-au-Prince, haitiPicha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Polisi hiyo imesema kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti unatuma onyo kali kwa viongozi wakuu wa magenge kusitisha vitendo vya uhalifu vya ubakaji, utekaji nyara, na mauaji.

Soma pia:Vifo vya genge lenye silaha Haiti vyafikia 109

Innocent amewekewa vikwazo na Marekani, Umoja wa Ulaya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku Marekani ikitoa zawadi ya dola milioni 2 kwa habari ztakazopelekea kukamatwa kwake. Amefunguliwa mashtaka nchini Marekani kwa utekaji nyara wa kutumia silaha wa wamisionari 16 wa Kikristo mnamo mwaka 2021 na kuuawa kwa mmishonari Marie Franklin na kutekwa nyara kwa mumewe mwaka 2022.