1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Myint Swe : Uasi unatishia kuisambaratisha Myanmar

9 Novemba 2023

Kiongozi wa serikali ya kijeshi nchini Myanmar amesema nchi hiyo iko katika hatari ya kusambaratika kutokana na kutoshughulilkiwa vizuri vurugu za hivi karibuni katika maeneo ya mpaka kati ya nchi hiyo na China

https://p.dw.com/p/4YcKR
Myint Swe akisoma ujumbe wa rais U Win Myint wakati wa shereza za maadhimisho ya miaka 71 ya uhuru wa Myanmar mnamo Januari 4, 2019
Rais wa baraza la utawala la Myanmar - Myint SwePicha: U Aung/Photoshot/Xinhua/IMAGO

Jeshi la Myanmar linakabiliwa na changamoto kubwa zaidi ya utawala wake tangu lilipochukuwa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka  2021, huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi kutoka kwa wanaharakati wanaopigania demokrasia na waasi wa makabila madogo kwenye ngome za jeshi hilo katika maeneo ya Kaskazini, Kaskazini mashariki, Kaskazini magharibi na Kusini Mashariki.

Myanmar haijashughulikia vizuri matukio katika mipaka yake

Rais wa baraza la utawala la nchi hiyo Myint Swe, ameuambia mkutano wa baraza la ulinzi na usalama wa taifa kwamba ikiwa serikali haitayashughulikia vizuri matukio hayo katika eneo la mpaka, nchi hiyo itagawika katika sehemu mbali mbali.

Soma pia:Kiongozi wa Myanmar asema uasi unatishia kulisambaratisha taifa

Swe amesema ni muhimu kudhibiti kwa uangalifu suala hilo kwa sababu sasa ni wakati muhimu kwa serikali ambapo inahitaji  raia  wote kuliunga mkono jeshi hilo.

Jeshi la Myanmar lajitaja kuwa taasisi ya kipekee ya kuleta utangamano

Kwa miongo kadhaa, jeshi hilo limesisitiza kuwa ndilo taasisi ya pekee yenye uwezo wa kuleta utangamano nchini humo na kutumia hoja hiyo kuhalalisha mkwamilio wake madarakani na kukandamiza upinzani.

Soma pia: Mungano wa makundi ya wanamgambo umesema mashambulizi yao yamenuia kuuangusha "utawala wa kidikteta" nchini Myanmar

Myanmar imekuwa katika machafuko tangu mapinduzi ya 2021 wakati majenerali wa kijeshi walipoiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia iliokuwa ikiongozwa na mwanaharakati wa demokrasia Aung San Suu Kyi, na kuhitimisha miaka 10 ya majaribio ya mageuzi baada ya miongo kadhaa ya utawala mkali wa kijeshi.

Kiongozi wa Myanmar aliyeondolewa madarakani kimabavu Aung San Suu Kyi akihudhuria mkutano na rais wa China Xi Jinping katika ikulu ya rais mjini Naypyitaw, Myanmar mnamo Januari 18, 2020
Kiongozi wa Myanmar aliyeondolewa madarakani kimabavu- Aung San Suu KyiPicha: Nyein Chan Naing/AP/picture alliance

Utawala wa kijeshi Myanmar wapoteza udhibiti wa baadi ya maeneo yake

Katika siku za hivi karibuni,  utawala wa kijeshi nchini humo umepoteza udhibiti wa baadhi ya maeneo ya miji katika mpaka wake na China kwa muungano wa makundi ya wapiganaji. Pia kumekuwa na ripoti nyingi za mapigano kwengineko kati ya wanajeshi na wapiganaji wa upinzani.  Hata hivyo vyombo vya habari havikuweza kuthibitisha ripoti hizo.

China yasema imepata majeruhi kutokana na mapigano Myanmar

Wiki hii, China ilithibitisha kwamba kumekuwa na majeruhi kutoka upande wake kutokana na risasi zilizofyatuliwa katika mapigano nchini Myanmar kuvuka upande wake wa mpaka . Hii leo, wizara ya mambo ya nje ya China, imewahimiza raia wake kujiepusha na maeneo yenye mapigano makali na kutosafiri kwenda Myanmar.

China yawataka raia wake Myanmar kuwa waangalifu

Katika taarifa, wizara hiyo imesema kuwa raia wa China ambao tayari wako katika maeneo yenye vurugu, wanapaswa kuwa waangalifu kutokana na hali hiyo na kuhamia maeneo salama ama kurejea nchini mwao. China ina maslahi makubwa ya kiuchumi nchini Myanmar.

Soma pia:China na Myanmar zasaka amani kufuatia ghasia za mpakani

Wakati wa ziara yake nchini Myanmar wiki iliyopita, naibu waziri wa mambo ya nje wa China, Nong Rong, aliitaka nchi hiyo kushirikiana na China kudumisha utulivu wa mpakani. Pia alitaka hatua kuchukuliwa kulinda maslahi ya China.