Kiongozi wa upinzani Chad auawa katika shambulizi
29 Februari 2024Msemaji wa serikali ambaye pia ni waziri wa mawasiliano Abderaman Koulamallah amesema Dillo alifariki jana, katika ofisi za chama chake ambako alikuwa amejifungia.
Hakutaka kujisalimisha na aliwafyatulia risasi askari. Mwendesha mashitaka mkuu awali alisema watu kadhaa wlaifariki akiwemo Yaya Dillo, bila kutoa maelezo ya mazingira ya vifo hivyo.
Dillo, ambaye alikiongoza chama cha upinzani cha Socialist Party Without Borders - PSF, alituhumiwa kwa kuongoza shambulizi kwenye ofisi za usalama wa ndani usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano.
Soma pia: Serikali ya Chad yatangaza tahadhari baada ya shambulizi kwenye idara ya usalama
Akizungumza na AFP jana, Dillo alikanusha kuhusika kwa vyovyote na tukio hilo, akiyataja madai hayo kuwa ni ya uwongo na yanayochochewa kisiasa.
Chad ilitangaza Jumanne kuwa uchaguzi wa rais utafanyika Mei 6, ambapo rais wa mpito Mahamat Idriss Deby Itno na Dillo ambaye ni binamu yake, walipanga kugombea.