Wataalamu wagunduwa kipande cha ndege MH370 Reunion
6 Agosti 2015Waziri wa usafiri wa Malaysia Liow Tiong amesema rekodi za matengenezo za shirika la ndege la Malaysia Airlines, zinathibitisha kuwa mabaki ya bawa la ndege lilogunduliwa wiki iliyopita ni la ndege iliyopotea ya shiriki hilo MH370.
Tiong amewaambia maripota kuwa timu ya Malaysia ambayo ni sehemu ya timu kubwa ya uchunguzi unaoendelea nchini Ufaransa, inauhakika kuwa kipande hicho cha bawa la ndege kinalingana na rekodi zao za matengenezo za ndege yao hiyo iliyopotea.
"Timu ya Malaysia iliyoko mjini Toulouse ambao kwa kweli ni wataalamu imethibitisha kuwa bawa la ndege lilopatikana ni la ndege ya MH370. Tunazishukuru mamlaka za Ufaransa kwa kutuunga mkono na kwa msaada wao waliotupa. Wakati huo huo tuheshimu uwamuzi wao wa kutaka kuendelea na uchunguzi zaidi. Lakini kwa upande wa timu ya uchunguzi ya Malaysia, ripoti ya kiufundi pamoja na ripoti ya matengenezo tulizonazo, tunaweza kuzitumia kulinganisha na kipande hicho cha mabaki ya bawa lilopatikana," anasema Liow Tiong. Ameongeza pia kuwa rangi ya bawa hilo inalingana na rekodi za shirika lao.
Mchambuzi wa sekta ya usafiri Henry H.Harttveldt amesema zaidi ya kipande kimoja kinahitajika ili kueleweka kilichoifika ndege hiyo MH370. Ameongeza kuwa kwa kawaida timu ya uchunguzi inatakiwa kutafuta data za usafiri wa ndege hiyo pamoja na kumbukumbu za sauti za marubani zilizorikodiwa, ili kupata maelezo zaidi ya kuweza kuwasaidia kugunduwa sabababu zilizoipelekea ndege hiyo kuanguka.
Waziri wa mambo ya nje wa China Hua Chunying amesema kuwa habari hizo mpya zilothibitishwa zinaashiria kuwa ndege hiyo ilianguka tu. Huku Caroline Sapriel mkurugenzi mtendaji wa shirika la CS&A la kutoa ushauri wa usiamamizi wa mifgogoro amesema, shirika la ndege la Malaysia litalazimika kuzungumza na familia za wote waliokuwa wamepanda ndege hiyo na kuwaeleza maendeleo ya uchunguzi wao. la sio hivyo shirika hilo la ndege linaweza kuzidi kuchafua jina lake.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/AP
Mhariri:Iddi Ssessanga