1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha UVIKO aina ya JN.1 kimeongezeka duniani

21 Desemba 2023

Huku msimu wa baridi kali ukiendelea barani Ulaya, virusi vya UVIKO aina ya JN.1 vinaongezeka katika nchi nyingi duniani.

https://p.dw.com/p/4aRxi
Symbolbild Coronavirus Selbsttest
Kifaa cha kupima UVIKO kwa haraka ambacho mtu anaweza kujipima mwenyewe.Picha: pressefoto_korb/picture alliance

Lakini hatari ya jumla kwa umma inatathminiwa kuwa chini, huku chanjo zilizopo zikiendelea kutoa ulinzi kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ujerumani imeshuhudia kuongezeka kwa viwango vya wagonjwa wanaolazwa hospitalini kutokana na maambukizi ya Uviko yanayohusiana na kirusi aina ya JN.1.

Soma pia: COVID-19 yarudi tena Ujerumani msimu wa baridi

Kulingana na takwimu rasmi, watu 302,100 nchini Ujerumani wameambukizwa kirusi hicho kufikia Desemba 20, idadi iliyoongezeka kutoka maambukizi 110,000 mnamo Oktoba 20 na 195,000 Novemba 20.

Rajib Dasgupta, mtaalam wa magonjwa katika Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, nchini India, amesema India pia inakabiliwa na hali mbaya ya maambukizi, haswa katika majimbo ya Kerala na Karnataka, ambapo viongozi wameimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kuwashauri watu kuchukua hatua zinazofaa.

Mtaalamu wa afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Washington huko St. Louis, Ziyad Al-Aly amesema hali hii sio tu kwa Ujerumani na India pekee, na kwamba hali inazidi kuwa mbaya na kirusi hicho kinaendelea kuenea duniani kote.

Hata hivyo viwango halisi vya maambukizo ya UVIKO vinauwezekano wa kuwa juu zaidi kuliko vile vinavyoripotiwa kwa sababu ya ukosefu wa upimaji.

Nchi nyingi ziliacha kuripoti utaratibu wa matokeo ya vipimo mwishoni mwa 2022 au mapema 2023, na kuna watu wachache tu ambao bado wanapimwa na vigumu kubaini idadi ya maambukizo kote ulimwenguni.

Umuhimu wa chanjo

 

Impfausweis und Nasenspray
Kadi ya chanjo pamoja na kichupa cha dawa ya kupuliza puani yenye nembo ya chanjo ya UVIKO.Picha: Ohde/Bildagentur-online/picture alliance

Al-Aly aliiambia DW kwamba ni muhimu sana kwa watu kupata chanjo mpya na pia kupata chanjo nyengine za kujikinga dhidi ya mafua. Na akaongezea kusema kwamba habari njema, ni kwamba chanjo za ziada zilizopo bado zinafaa dhidi ya kirusi cha JN.1.

Soma pia: Utafiti: Watu 476 walifariki kutokana na UVIKO-19 Tanzania

Hata hivyo, chanjo za kuimarisha kinga hazipatikani kila mahali duniani, alisema Dasgupta: "India imesitisha chanzo hizo. Kwa hakika, utoaji wa dozi ya tatu ya nyongeza umekuwa nyuma sana ya dozi mbili za kwanza."

Vile vile kutokana na hali hii Shirika la Afya Ulimwenguni WHO linapendekeza kuvaa barakoa katika maeneo ya umma au kuepuka mikusanyiko ya kijamii ikiwa unajihisi mgonjwa ili kusaidia kupunguza kuenea kwa virusi.