1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kituo cha polisi chavamiwa pwani ya Kenya

23 Desemba 2016

Watu wenye mishale, pinde na mapanga, wamekivamia kituo kimoja cha polisi katika pwani ya Kenya, katika mapambano ambayo yamewajeruhi maafisa watatu na kumuua mshambuliaji mmoja.

https://p.dw.com/p/2Un4L
Kasino Überfall Mombasa Republican Council MRC Kenia Afrika
Picha: Reuters

Kamishna wa polisi wa Kaunti ya Kwale, Kutwa Olaka, ameliambia shirika la habari la Reuters, kwamba washambuliaji wapatao 10, walikivamia kituo cha polisi cha Kombani, kilicho umbali wa kilomita 20 kusini mwa mji wa Mombasa, majira ya saa tisa alfajiri ya leo (Ijumaa, 23 Disemba).

Bado kundi hilo la washambuliaji halifahamiki lililokotokea.

Kombani ni ngome ya Baraza la Jamhuri ya Mombasa, MRC, kundi ambalo limepigwa marufuku nchini Kenya kwa kupigania uhuru wa upwa wa Kenya, likidai kudharauliwa kwa eneo hilo na serikali kuu ya Nairobi.

Katika mwaka 2013, kundi hilo lilidaiwa kupanga na kuhusika kwenye mashambulizi kadhaa dhidi ya vituo vya polisi kwenye eneo la pwani.