Kodi mpya ya miamala Tanzania yawatia wananchi wasiwasi
15 Julai 2021Hofu hiyo inakuja kutokana na gharama zake kuonekana kuwa mzigo kwa wananchi na hasa wakati ambako kunashuhudiwa kupanda kwa gharama nyingine za maisha kulikosababishwa na ongezeko la kodi katika nishati ya mafuta ya diesel na petrol.
Kwa mfano kwa kuangalia ukokotoaaji wa tuzo hizo, mtu aliyekuwa akipokea fedha kiasi cha shilingi 100,000 kutoka kwa wakala alikuwa akikatwa kiasi cha 3,600, sasa atakuwa akikatwa jumla ya shilingi 6,100 na kiwango hicho kinazidi kupanda kadri muamala wa fedha unavyoongezeka.
Lakini jambo linaloonekana kuwaumiza wananchi zaidi ni lile la makato hayo kufanyika zaidi ya mara mbili, yaani mtumaji na mtumiwaji. Hali hii ni tofauti na ilivyokuwa imezoeleka hapo nyuma wakati ambapo makato ya fedha yaliyokuwa yakifanyika kwa mpokeaji wa fedha pekee lakini sasa tuzo hiyo inakula pande zote mbili.
Kila anayepewa nafasi kuzungumzia kuhusiana na tuzo hiyo, hapishani sana na mwenzake, wote wakionyesha vilio vyao.
Tuzo hizo zinaonekana kuwazidisha wasiwasi kwa wananchi wanaohofia siyo tu uwezekano wa kupanda kwa gharama za maisha bali pengine kuanguka katika shughuli zao kutokana kuwabana watu wa kipato cha aina yoyote.
Licha ya kilio cha wengi, Serikali inaonekana kukaza kamba ikisistiza kuwa hakuna namna nyingine mbali ya tuzo hiyo kuanza kutozwa leo Julai 15 na kuendelea.
Soma pia: Makampuni ya kigeni yalalamikia kodi kubwa Tanzania
Hatua hiyo ya serikali siyo tu inaacha hofu kwa watumiaji wa huduma za simu za mikoni lakini pia inaibua wasiwasi mwingine juu ya majaliwa ya mitandao hiyo kuendelea na kushamiri huku wengi wakihofu kuwa pengine watumiaji wakatafuta njia nyingine mbadala kama vile huduma za kibenki.
Mtaalamu wa masuala ya fedha kutoka Chuo Cha Usimamizi wa fedha IFM, Profesa Bill Kiwia amesema ongezeko hilo la kodi litaleta athari za moja kwa moja kwa wananchi.
Katika miaka ya hivi karibuni kiwango cha matumizi ya simu za mikononi kimekuwa kikiongezeka na ongezeko hilo linashuhudiwa pia katika maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme imeanza kuimarika.
Kuwepo kwa kodi hiyo pengine kukawa ni pigo kubwa kwa wananchi hao wa vijijini ambako huduma za simu za mikononi kwao siyo jambo la anasa bali ni nyenzo muhumu inayotumika kuendesha maisha kama vile kusaka masoko ya mazao yao.