1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Dunia: Brazil na Ureno zafuzu duru ya mtoano

Daniel Gakuba
29 Novemba 2022

Brazil na Ureno zimefuzu kuingia katika duru ya mtoano ya 16 bora katika mashindano ya Kombe la Dunia baada ya kupata ushindi katika mechi zilizochezwa jioni ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4KCzL
Fußball-WM Katar 2022 | Brasilien v Schweiz
Picha: CARL RECINE/REUTERS

 

Brazil ambayo ilicheza bila nyota wake Neymar ilimudu kuishinda Uswisi goli moja kwa sufuri na kuandikisha ushindi wa pili baada ya kuilaza Serbia kwa magoli mawili kwa sufuri kwenye mechi ya kwanza.

Kocha wa Brazil, Tite amekiri kuwa pengo la Neymar lilionekana, ingawa wanao wachezaji wengi mahiri wanaoweza kuokoa jahazi kama ilivyotokea dhidi ya Uswizi, ambayo ilitoa upinzani mkali.

Soma zaidi: Cameroon yaweka hai matumaini yake Kombe la Dunia

Bao la Brazil ambalo lilikuwa pekee katika mechi hiyo ya kuvutia lilitiwa kimiani na mchezaji wa katikati Casemiro mnamo dakika ya 83 ya mchezo, kwa kombora kali ambalo lilimuacha kipa wa Uswisi Yann Sommer akisimama kama mtazamaji.

Casemiro alisema walijua bila Neymar haitakuwa kazi mteremko, na kuongeza kuwa kilicho muhimu ni kwamba lengo lao la kufuzu kwa ngazi inayofuata limetimia.

FIFA Fussball-Weltmeisterschaft Katar 2022 – Gruppe H – Portugal – Uruguay
Bruno Fernandes aling'ara katika mechi dhidi ya UruguayPicha: Lee Smith/REUTERS

Ureno yalipiza kisasi dhidi ya Uruguay

Katika mechi ya mwisho jana, Ureno ya Cristiano Ronaldo iliikandamiza Uruguay kwa kuibamiza magoli mawili bila majibu, mara mbili zote nyavu zikitikiswa na Bruno Fernandes.

Soma zaidi: Kocha wa Ghana alalamikia Penalti ya Ronaldo

Kwa karibu kipindi chote cha mchezo Ureno ilikuwa timu bora, ikiliona lango kwa mara ya kwanza katika dakika ya 54 ya mchezo kupitia krosi iliyomiminwa na Bruno Fernandes ambayo alikamilisha kazi kwa mkwaju wa penalti katika dakika za nyongeza.

Uruguay ambayo iliitoa Ureno katika kombe la dunia la mwaka 2018, itapambana na Ghana katika mechi ya mwisho, zote mbili zikitia matumaini katika kuishinda mechi hiyo, na kisha kutegemea Ureno kuicharaza Korea Kusini.

Fußball-WM Katar 2022 | Südkorea v Ghana
Nyota ya kijana Mohammed Kudus wa Black Stars iliangaza kwa kupachika magoli mawili dhidi ya Korea KusiniPicha: KAI PFAFFENBACH/REUTERS

Timu za Afrika zajikakamua

Mechi mbili za mapema jana ziliwafurahisha mashabiki wa soka barani Afrika. Ya kwanza, japo Kameruni haikupata ushindi ilipambana vikali kutoka kichapo cha magoli matatu kwa moja dhidi ya Serbia na kusawazisha katika mojawapo ya mechi bora kabisa za mashindano haya.

Soma zaidi: Michuano ya Kombe la Dunia 2022 yazinduliwa rasmi

Kisha Ghana ilizikosha nyoyo za mashabiki wake kwa kuondoka na ushindi wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya timu jeuri ya Korea Kusini.

Leo hii zinachezwa mechi za mwisho katika makundi A na B. Katika kundi A Senegal ina miadi na Ecuador huku Uholanzi ikiminyana na mwenyeji Qatar ambayo tayari ilikwiyaaga mashindano. Mechi zitachezwa kwa wakati mmoja saa kumi na mbili Afrika Mashariki.

Saa nne usiku Afrika mashariki Iran itakabana na Marekani, huku England na Wales zikipambana katika dabi ya kisiwa cha Uingereza.

-ape, rtre