Uhispania na Japan zafuzu hatua ya 16 bora Kombe la Dunia
27 Julai 2023Michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake la mwaka 2023 bado inaendelea kutifua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini Australia na New Zealand ambapo kwa sasa michuano hiyo imefikia katika hatua muhimu ya kuamua hatma za timu zinazoshiriki.
Soma zaidi: Kombe la Dunia: Afrika Kusini na Zambia zapokea kichapo
Timu 16 zitatinga hatua ya mtoano ndani ya siku chache zijazo, huku nyingine zikiyaaga michuano hiyo moja kwa moja kutoka hatua ya makundi.
Hadi kufikia sasa timu za Uhispania na Japan za kundi C ndio zimefanikiwa kutinga katika hatua ya 16 bora ingawa msimamo kamili wa kundi C utaaamuliwa katika mechi ya mwisho itakayokutanisha timu hizo mbili.
Timu ya taifa ya Marekani ilikuwa inapewa nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora kabla ya mchezo wao wa leo dhidi ya Uholanzi uliotamatika kwa sare ya kufungana goli moja kwa moja na kuifanya sasa kusubiri mechi ya mwisho watakapocheza na Ureno ambao wameshinda mechi yao dhidi ya Vietnam kwa goli 2-0.
Kundi E litasubiri hadi mechi zao za mwisho kuamua ni nani atakayetinga hatua ya 16 bora. Marekani inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 4, sawa na Uholanzi huku Ureno ikishikilia nafasi ya tatu ikiwa na alama 3.
Timu zilizotolewa katika hatua ya makundi
Hadi kufikia leo timu zilizotolewa katika mashindano hayo ya Kombe la Dunia la wanawake 2023 ni Zambia, Jamhuri ya Ireland na Costa Rica na kilichobaki ni kukamilisha tu ratiba na kufungasha virago kurudi nyumbani.
Timu ya taifa ya Nigeria itakuwa na kibarua cha kuhakikisha inapata alama tatu mbele ya wenyeji Australia hapo baadae. Vipusa wa Nigeria wanahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini yao ya kutinga hatua ya 16 bora.
Nigeria imetulia katika nafasi ya tatu ikiwa na alama moja kuelekea mchezo wa leo, wakati Australia iko katika nafasi ya pili na alama tatu.
Canada inaongoza kundi B na alama nne huku Jamhuri ya Ireland ikiburuta mkia wakati hatma yao ikiwa tayari imeamualiwa.