Kongamano la kimataifa la Uchumi lafunguliwa Davos
20 Januari 2016Wajumbe 2500 kutoka zaidi ya mataifa 100,wakiwemo wakuu wa makampuni 1500 na zaidi ya viongozi 50 wa taifa na serikali wanahudhuria kongamano hilo la siku nne linaloitishwa kila mwaka ,linaloanza rasmi leo na kuendelea hadi jumamosi ijayo.
Wajumbe wanakabiliana na ulimwengu unaozidi kugawika,idadi ya maskini ikizidi kuwa kubwa kulinganishwa na matajiri pamoja pia na kuzidi kupanuka nyufa za kisiasa nchini Marekani,Ulaya na mashariki ya kati,hali ambayo haijawahi kushuhudiwa wakati wowote ule tangu miongo kadhaa iliyopita.
Pengo kati ya maskini na Matajiri linazidi kupanuka
Shirika la kimataifa linalopambana dhidi ya umaskini ulimwenguni,Oxfam limetoa ripoti inayoonyesha asili mia moja ya watu ulimwenguni wana miliki utajiri unaopindukia uwezo wa fedha walizonazo asili mia 99 ya waliosalia.
Kwa maneno mengine pengo upande huo linapanuka kuliko wakati wowote ule mwengine.
Mizozo pia imeenea barani,na kusababisha mwanya mpana wa kinadharia kuhusu jinsi ya kuushughulikia mzozo mkubwa kabisa wa wakimbizi kuwahi kushuhudiwa tangu vita vikuu vya pili kumalizika,huku Uingereza ikitishia kujitoa katika Umoja wa Ulaya na kuzusha hofu kuhusu mustakbal wa miongo mitano ya juhudi za kuzidi kuileta pamoja jumuia hiyo.
Akifungua kongamano hilo,mwenyekiti na mwasisi wa kongamano la kiuchumi la kimataifa mjini Davos, Klaus Schwab hakuitaja mizozo inayoikabili dunia badala yake ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa majadiliano na ushirikiano akisifu zaidi mchango jumla wa viongozi vijana:
"Tumefika hapa kuwakilisha watu wa tabaka zote,viongozi wa kisiasa,wafanyabiashara au washirika na wanachama wetu,lakini pia ningependa kuwakaribisha wawakilishi wa mashirika ya kiraia,na hasa vijana.Tunaamini vijana wa rika ya miaka 27 wa dunia wanabidi wawajibike pia. Kwa hivyo nawakaribisha zaidi viongozi wetu vijana,wabunifu wetu na wajasiria mali wetu wa jamii.“
Hatua za usalama zimeimarishwa Davos
Waandalizi wa kongamano hilo la kimataifa wameimarisha hatua za ulinzi ili kupunguza hatari ya kutokea mashambulio.
Mbali na masuala ya kiuchumi, na wimbi la wakimbizi,juhudi za kupambana na wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam ni miongoni mwa mada katika kongamano la mwaka huu.
Miongoni mwa viongozi wanaohudhuria kongamano la kimataifa la kiuchumi ni pamoja na makamo wa rais wa Marekani Joe Biden na waziri wa mambo ya nchi za nje John Kerry,waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran na Saud Arabia.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga