1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroJamhuri ya Kongo

Kongo: Mji wa Sake haujadhibitiwa na waasi

Hawa Bihoga
14 Februari 2024

Mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 yanaendelea karibu na mji wa kimkakati wa Sake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kusababisha watu kuyakimbia makaazi yao.

https://p.dw.com/p/4cNtl
DR Kongo I Waasi wa M23
Wapiganaji wa waasi wa M23 wakiwa katika oparesheni zaoPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Mapigano yameshuhudiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni yakizunguka mji huo wa kimkakati, ambao uko umbali wa kilometa 20 kutoka katika mji wa Goma, ambo ni mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini.

Wakaazi wa mji huo walisema kuwa mapigano hayo ambayo yanaongeza hali ya wasiwasi yaliendelea kwenye vilima vinavyozunguka mji wa eneo hilo.

Baada ya makabiliano makali siku ya Jumatatu afisa wa masuala ya usalama ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "licha ya mapigano kuendelea, bado Sake ipo chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali." Afisa huyo aliongeza kuwa mapigano bado yaliyokuwa yakiendelea kuwafurusha wapiganaji wa M23, waliokuwa wakijaribu kujipenyeza katika mji huo.

Wakati hali hiyo ikishuhudiwa Meya wa mji huo Maombi Mubiri alisema kuwa watu wamekimbia makaazi yao katika mji huo kutokana na hofu ya mapigano yanayoendelea.

Meya Maombi aliongeza kuwa kwa sasa waasi wa M23 wanadhibiti sehemu ya kusini mwa mji, "Wanamgambo wanaounga mkono serikali (wazalendo) wapo katika eneo la kaskazini mwa mji huo."

Soma pia:Waasi wa M23 wauzingira mji wa Sake, DRC

Mmoja wa maafisa afya katika eneo hilo ambaye pia hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la AFP kwamba milio ya risasi ya hapa na pale ilisikika na watu watatu walijeruhiwa na kupatiwa matibabu ya awali na baadaye kuhamishiwa katika mji wa Goma, kutokana na hali zao kutoridhisha.

Kundi la M23 lenye idadi kubwa ya wanachama wenye asili ya Watutsi limeteka maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini tangu lilipotoka katika hali ya utulivu mwishoni mwa 2021, katika eneo lililokumbwa na ghasia kwa miongo kadhaa kufuatia vita vya kikanda katika miaka ya 1990.

Waziri wa Ulinzi wa Kongo Jean-Pierre Bemba, katika ziara yake ya pili mjini Goma chini ya wiki moja, alitoa hakikisho kwamba "kila kitu kinafanyika kulinda watu wa Sake, Goma na maeneo jirani".

Waziri Bemba aliongeza kwamba serikali ya mjini Kinshasa inakusudia "kuchukua tena udhibiti wa maeneo yote" waliopoteza baada ya waasi wa M23 kuyatwaa kufuatia mapigano makali.

Wasiwasi wa UN kufuatia mapigano mashariki mwa Kongo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mapema juma hili lilielezea wasiwasi wake kufuatia "kuongezeka kwa ghasia" mashariki mwa Kongo na kulaani mashambulizi ya waasi yaliyoanzishwa karibu na mji wa Goma mnamo Februari 7.

Umoja wa Mataifa | Baraza la Usalama
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika vikao vyakePicha: DAVID DEE DELGADO/REUTERS

Kwa mujibu wa waraka wa Umoja wa Mataifa, jeshi la Rwanda linatumia silaha za kisasa kama vile makombora ya kutoka ardhini hadi angani kusaidia M23 kwenye mashambulizi yake.

Waraka huo wa siri ulisema kuwa "kombora linaloshukiwa kuwa la Jeshi la Ulinzi la Rwanda, RDF, likitokea ardhini hadi angani lilirushwa kuelekea kwenye droni ya uangalizi ya Umoja wa mataifa siku ya Jumatano, lakini halikufanya uharibifu wowote.

Hali hiyo imeongeza mvutano kati ya serikali ya Kinshasa na Kigali, baada ya Kongo kuendelea kuishutumu serikali ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23.

Soma pia:Baraza la Usalama lahofia "kutanuka ghasia" Kongo Mashariki

Kongo, Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zinasema Rwanda inaunga mkono waasi katika jitihada za kudhibiti rasilimali nyingi za madini, madai ambayo Kigali inayakanusha.

M23 inasema inatetea watu wachache wanaotishiwa na inataka mazungumzo na serikali ya Rais Felix Tshisekedi, ambayo inakataa kuzungumza na kile inachoita "magaidi".

Kumekuwepo na mkururo wa juhudi za kidiplomasia kusitisha mapigano hadi sasa, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa kufikia lengo la suluhu la kudumu.

Siku ya Jumanne, Burundi ilitangaza kuwa Rais Evariste Ndayishimiye atazuru Kongo "katika mfumo wa mashauriano" kwa ajili ya makubaliano ya amani ya kikanda.

Mashambulizi ya kushtukiza katika mji wa Sake, Kongo