1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaanzisha kampeni ya chanjo ya Ebola

18 Februari 2021

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeanzisha kampeni ya chanjo dhidi ya homa ya Ebola katika mji wa Butembo, ambako wagonjwa wa Ebola walipatiwa matibabu kabla ya kugunduliwa walikuwa wanaugua ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/3pXmA
Ebola-Impfung in Liberia 02.02.2015
Picha: Reuters/J. Giahyue

Kampeni hii ya chanjo dhidi ya homa ya Ebola imeanzishwa ili kuzuwia kusambaa zaidi kwa homa hii kali, baada ya ugonjwa huo kuzuka upya katika wilaya ya Lubero kusini mwa mji wa Butembo.

Akuzungumza na waandishi habari katika mji wa Butembo aliko hivi sasa kusimamia shughuli za kukabiliana na Ebola, Waziri wa Afya katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Dokta Nzanzu Syalita Eugène alisema licha ya wakaazi waliokutana na wagonjwa wa Ebola kukubali kupewa chanjo na nyumba zao kusafishwa, kuna sehemu ambako mtu mmoja aliwatolea vitisho wataalamu wa afya.

Wakati akitangaza kuanzishwa kwa kampeni hiyo ya chanjo dhidi ya Ebola, Waziri Nzanzu Syalita anasema kwamba dawa za kuwatibu wagonjwa wa Ebola zimewasili tayari Butembo.

Weltspiegel 16.02.2021 | DR Kongo | Ebola, Quarantäne-Areal Matanda Hospital
Mfanyakazi wa afya akikagua hospitali ya Matanda, Butembo ambako mgonjwa wa kwanza wa ebola alifarikiPicha: Al-hadji Kudra Maliro/AP Photo/picture alliance

Ebola ikiwa iliwauwa watu wengi katika eneo hili, ilipozuka homa hiyo mnamo mwaka wa 2018, idadi kubwa ya wakaazi wa eneo linaloshuhudia homa ya Ebola kwa sasa wamekubali kuheshimu kanuni za usafi, na kupata chanjo ili kuepukana na maambukizi mapya.

Soma zaidi: Kongo yarekodi kisa kipya cha Ebola

Tangu kuzuka kwa homa ya Ebola katika wilaya ya Lubero pamoja na mji wa Butembo, ni watu wanne hadi sasa walioambukizwa, na wawili kati yao wameshafariki dunia, na wawili wanaendelea kupatiwa matibabu katika vituo vya afya.

Mripuko wa homa ya Ebola katika wilaya ya afya ya Masoya huko Lubero, ni wa 12 kushuhudiwa katika nchi hii, baada ya ule wa Équateur.

Kinachotakiwa kwa wakaazi wa eneo hili ni kuheshimu kanuni za usafi, ili kuitokomeza homa hii, inayotokea, wakati Kongo ikiendelea pia kupambana na janga la virusi vya corona.