Kongo yasema imejiandaa vyema kwa uchaguzi wa Jumatano
18 Desemba 2023Tume ya uchaguzi CENI, imeelezea utayari wake wa kufanyika uchaguzi kote nchini Kongo hapo Jumatano, na kusema vifaa vya uchaguzi ikiwemo karatasi za kura na fomu za kuorodhesha matukio ya uchaguzi katika kila kituo cha kupigia kura vimewasili nchini humo na kusambazwa kwenye mikoa yote ishirini ya sita.
‘‘Niwathibitishie kwamba kila kitu kinafanywa ili uchaguzi wa hapo Desemba 20 ufanyike. Kuna vifaa vya uchaguzi kama vile mashine ya kupigia kura tayari vimetawanywa kote nchini.
Tumepata ndege za mizigo na helikopta ambazo zimeendelea kupeleka vifaa vingine kwenye maeneo mablimbali" alisema Patiricia Nseya, msemaji wa CENI, na kuongeza kuwa changamoto za usambazaji wa vifaa hivyo zitatatuliwa.
Soma pia: Kampeni za uchaguzi nchini Kongo zinakamilika rasmi leo Jumatatu
Tume ya uchaguzi imesema vifaa vya uchaguzi kwenye jimbo la Ituri huko kaskazini -Mashariki mwa nchi vimetawanywa kwa salimia tisini na tisa kwa msaada wa ndege za kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, Monusco.
Serikali ya Kongo imetangaza jana kwamba imepokea ndege mbili za mizigo kutoka kwa jeshi la Misri ili kusafirisha vifaa vya uchaguzi.
Changamoto ya miundombinu duni
Kongo ambayo haina miundombinu za barabara inategemea kwa asilimia kubwa usafiri wa ndege. Na kumekuwa na wasiwasi kwamba vifaa vya uchaguzi huenda vikachelewa kufikishwa kwenye vituo vyote 75.000 vya kupigia kura ifikapo Jumatano.
Huku hayo ya kiendelea, wagombea wa Urais wanatoa nguvu zao za mwisho katika kampeni ambayo itamalizika usiku wa leo. Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili, ataitimisha kampeni yake hapa mjini Kinshasa ambapo atakuwa na mkutano wa hadhara.
Soma pia: DRC yahesabu siku kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumatano
Na kampeni ya lala salama ya mpinzani Moise Katumbi itafanyika leo huko Kananga Jimboni Kassai ambapo ndio ngome ya rais wa sasa. Kwa ujumla kampeni hiyo iliodumu siku salathini ilifanika kwa utulivu licha ya vurugu za hapa na pale. Duru za kiusalama zimesema angalau watu wawili waliuwawa katika vurugu hizo.
Wakati huohuo waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika wamewasili hapa nchini. Ujumbe huo wa watu 80 umetarajiwa kutawanywa katika maeneo kadhaa ya nchi.
Waangalizi hao wamekuja baada ya wale wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC na pia wale wa kituo cha Carter Center kutoka Marekani.
Kwa upande wake Umoja wa Ulaya uliondoa waangalizi wake baada ya serikali ya Kongo kutoruhusu kuingia nchini baadhi ya vifaa vya mawasiliano vya ujumbe huo.