DRC yasikitishwa na unyanyasaji dhidi ya wanadiplomasia
27 Agosti 2024Mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimezungumzia masikitiko yake kuhusiana na tukio la kunyanyaswa kwa wanadiplomasua watatu wa Ufaransa mjini Kinshasa.Vyanzo vya serikali na kidiplomasia ndivyo vilivyotoa taarifa hiyo kwa shirika la habari la AFP.
Taarifa ya wizara ya sheria ya Kongo imesema maafisa wa polisi walikuwa miongoni mwa kundi lilikovamia eneo la ofisi linatumiwa na ubalozi wa Ufaransa kwa lengo la kutaka kumuondoa kwa nguvu balozi wa Ufaransa.
Soma: Ziara ya Rais wa zamani wa Ufaransa yazua gumzo Kongo
Chanzo cha kidiplomasia kimefahamisha kwamba,mwanadiplomasia anayehusika na ushirikiano wa masuala ya utamaduni wa Ufaransa alishikiliwa kwa takriban masaa matatu wakati wanadiplomasia wengine wawili walihangaishwa. Maafisa wa polisi na ofisi ya mwendesha mashtaka wamehusishwa na unyanyasaji huo na baadhi yao wameshakamatwa kwa mujibu wa wizara ya sheria ya Kongo. Mahakama moja nchini Kongo mwaka jana ilitowa uamuzi ulioipa Ufaransa uhalali wa kumiliki eneo la ofisi linalozozaniwa ambako ndiko uliko ubalozi wa Ufaransa tangu mwaka 1972. Jana Jumatatu balozi wa Ufaransa Bruno Aubert alikutana na rais Felix Tshisekedi kuhusiana na suala hilo.