Kongo yazindua kampeni ya kiti kwenye Baraza la Usalama UN
19 Desemba 2024Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo Therese Kayikwamba Wagner aliwaambia wanadiplomasia na maafisa wa Kongo katika hafla hiyo Jumatano kwamba iwapo taifa lake litachaguliwa litafanya juhudi za kushawishi mjadala wa ulinzi wa amani na mageuzi ya kujenga amani, pamoja na mageuzi ya mfumo wa usalama wa pamoja wa Umoja wa Mataifa.
Baraza la Usalama lina jukumu la kudumisha amani na usalama wa kimataifa, na linaweza kuchukua maamuzi ya kisheria, kuidhinisha matumizi ya nguvu, na kuweka vikwazo.
Linaundwa na wanachama watano wa kudumu -- China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani, na wanachama 10 wasio wa kudumu ambao wanachaguliwa kwa mihula ya miaka miwili na Baraza Kuu lakini hawana uwezo wa kura ya turufu.
Nchi hiyo ya Afrika ya kati imechaguliwa mara mbili kuwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa -- mwaka 1982-1983, na 1991-1992 wakati wa Vita vya Ghuba.