1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroKorea Kaskazini

Korea Kaskazini yafanya tena luteka jirani na eneo la mzozo

6 Januari 2024

Korea Kaskazini imefanya luteka nyingine leo kwa kufyetua makombora karibu na eneo la mpaka wa bahari unaozozaniwa kati yake na taifa jirani la Korea Kusini.

https://p.dw.com/p/4avgk
Luteka ya Korea Kaskazini ya siku ya Ijumaa, Januari 5, 2024.
Luteka ya Korea Kaskazini ya siku ya Ijumaa, Januari 5, 2024.Picha: Jung Yeon-je/AFP

Taarifa ya jopo la wakuu wa vikosi vya ulinzi vya Korea Kusini imesema Pyongyang imefyetua zaidi ya makombora 60 karibu na mpaka wa bahari wa magharibi siku moja baada ya kufanya luteka kama hiyo kwa kurusha kiasi makombora 200 kwenye eneo hilo.

Korea Kusini ilijibu kitendo hicho cha jana Ijumaa kwa yenyewe kufyetua mizinga ipatayo 400 kutokea upande wa kusini wa eneo la mpaka wenye mzozo.

Hii leo serikali mjini Seoul imetoa mwito kwa Korea Kaskazini kukomesha matendo yote yanayoongeza mivutano lakini imeonya kwamba haitasita kujibu kwa hatua tabia za uchokozi kutoka Pyongyang.

Korea Kaskazini imesema mazoezi yake ya kijeshi ni jibu kwa luteka iliyofanywa na Korea Kusini mapema wiki hii.