1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Korea Kusini kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Yoon

13 Desemba 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Korea Kusini amewatolea wito wabunge wa chama tawala kuungana na wananchi katika azma ya kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol kutokana na kutangaza kwake sheria ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/4o7Xw
rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol alipotangaza sheria ya kijeshi
Rais Yoon alijikuta kwenye msukosuko wa kisiasa baada ya kutangaza sheria ya kijeshi ambayo baadaye aliondoa lakini ilighadhabisha wengi nchini mwakePicha: YONHAP/REUTERS

Wito huo wa  kiongozi wa chama cha Democratic, Lee Jae-myung, unatolewa siku moja kabla ya kura ya pili ya bunge ya kutokuwa na imani na rais huyo itakayofanyika Jumamosi jioni, ambayo hata hivyo matokeo yake hayatabiriki.

Kura mia mbili zinahitajika ili hatua hiyo ipitishwe, ikimaanisha kuwa wabunge wa upinzani wanatakiwa kuwashawishi wabunge wanane wa chama tawala cha People Power Party (PPP) kujiunga nao.

Kufikia Ijumaa mchana, wabunge saba wa chama tawala walikuwa wameahidi kuunga mkono kura hiyo.

Jaribio la kwanza la kumwondoa Rais Yoon lilishindikana na hivyo taifa hilo kuendelea kuwa kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa.