Korea Kusini yavutiwa na Ujerumani kama mfano wa muungano
3 Oktoba 2021Ujerumani inaadhimisha Jumapili hii ya tarehe 03.10.2021 miaka 31 ya kumbukumbu ya muungano kati ya upande wake wa Magharibi na iliyokuwa Ujerumani Mashariki.
Korea Kusini inaitazama Ujerumani kama mfano. Wakati wajerumani wakiadhimisha kumbukumbu hiyo ya miaka 31 ya muungano Korea Kaskazini na Kusini bado ziko kwenye mvutano kuhusu suala la kuunganisha rasi yao hiyo na namna gharama ya kuijenga upya Kaskazini itakavyopatikana.
Ikiwa ni miezi saba tu iliyobakia kabla ya rais wa Korea Kusini Moon Jae in na serikali yake kuondoka madarakani, kiongozi huyo na serikali yake bado wanaipigania ndoto yao ya muda mrefu ya kutaka kuona Korea mbili zinaungana na kuwa taifa moja.
Na Ujerumani kama moja ya nchi chache ambazo ni mifano ya hivi karibuni yenye uzoefu wa mtengano wa nchi mbili na baadae kuungana,waziri wa muungano wa Korea Kusini, Lee In Young anakwenda barani Ulaya kuzungumzia kile ambacho wanaweza kujifunza kutokana na matukio yaliyopelekea Ujerumani kuungana mnamo mwaka 1990 na yaliyojitokeza baadae.
Wachambuzi wanasema kwamba rais Moon na waziri wake wa masuala ya muungano, Lee wamechoswa na kukasirishwa na hatua ya kushindwa kuisogeza mbele ajenda yao ya kutaka kuzileta karibu Korea hizo mbili katIka kipindi cha miaka mitano iliyopita.Lakini wanasema kwamba sababu ya kuwepo kwa mivutano katika uhusiano wa pande hizo mbili haitokani na Korea Kusini.
Hatua ya serikali ya mjini Pyongyang ya kukataa kukataa kubadili mtizamo na kukataa hata kuwa na mawasiliano na serikali ya mjini Seoul kwa sehemu kubwa ya mwaka uliopita, kumechangia kusimamisha uhusiano baina ya pande hizo mbili,uhusiano ambao toka hapo una mashaka. Na upande wa Kaskszini wiki za hivi karibuni ulipochukua juhudi za kujaribu kujisogeza tena, iliyavuruga zaidi mambo ilipoamua kufanya msururu wa majaribio ya makombora. Mnamo siku ya Ijumaa Korea Kaskazini ilithibitisha kwamba ilijaribu kombora lake jipya la kuharibu ndege siku ya alhamisi wakati ambapo Jumanne ilizindua silaha ambayo serikali hiyo iliielezea kuwa ni kombora lililotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ya kijeshi lenye uwezo wa hali ya juu. Marekani na Japan ziliilaani hatua hiyo ya Kaskazini zikisema kilichofanywa na nchi hiyo ni ukiukaji wa maazimio kadhaa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Bado lakini ndoto ya muungano inabakia kuwa matarajio ya muda mrefu. Waziri anayehusika na masuala ya muungano kutoka upande wa Kusini Lee alianza ziara barani Ulaya Jumatano akipanga kuwa na mazungumzo na maafisa wa serikali za Ubelgiji, na Sweden kabla ya kwenda Ujerumani.
Lee amealikwa na bunge la Ujerumani kuhudhuria sherehe za kumbukumbu ya miaka 31 ya muungano wa Ujerumani leo Jumapili. Jana Jumamosi alizungumza katika chuo kikuu huria cha Berlin kuhusu uhusiano wa Korea mbili na Jumatatu atakutana na rais wa shirikisho Frank Walter Steinmeier kujadili uzoefu iliyoupitia Ujerumani kabla na baada ya muungano wao na uwezekano uliopo wa hilo kufanyika katika rasi ya Korea.
Ingawa wachambuzi wanasema kwamba Ujerumani ilikabiliwa na vizingiti vikubwa mnamo 1990 na vingine vingi ambavyo haikuvitarajia katika miaka iliyofuatia mara baada ya muungano wa Mashariki na Magharibi, hali katika Korea mbili inaonesha wazi kabisa kwamba ni ngumu zaidi. Na moja ya tatizo kubwa ambalo inabidi litatuliwe ni kwamba bado Korea Kaskazini inajitazama kama ndio utawala pekee halali kwenye rasi hiyo, na kipindi chote imesisitiza kwamba muungano wowote utakaofikiwa hapo baadae utalazimika kukamilika chini ya maelekezo na muongozo wake.