1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuachiliwa huru mahabusu wa Kijerumani katika Milima ya Uturuki

Othman, Miraji21 Julai 2008

Wajerumani watatu waachwa huru Uturuki bila ya damu kumwagika

https://p.dw.com/p/EgLh
Maandamano ya Chama cha PKK cha Wakurd katika jiji la BerlinPicha: AP

Mkasa wa kutekwa nyara Wajerumani watatu waliokuwa wanapanda milima huko Ararat, nchini Uturuki, umemalizika bila ya kumwagika damu. Watu hao waliotekwa nyara na wapiganaji wa Chama cha Wakurd cha PKK kilichopigwa marufuku huko Uturuki na kuachwa huru jana, walikuwa mahabusi kwa siku kumi na mbili. Gerwald Herter anauelezea mkasa huo katika uhariri ufuatao, ukisomwa studioni na Othman Miraji...


Chama cha PKK si tu hakijaitathmini vizuri hali ya mambo, lakini kimejiharibia zaidi hali yake, tena bila ya kulazimika kufanya hivyo. Na zaidi kimefanya hivyo kwa gharama ya mahabusi hao wa Kijerumani na familia zao. Kutokana na operesheni za jeshi la Uturuki huko Kaskazini mwa nchi hiyo, wapiganaji wa Chama cha Wakurd cha PKK wamedhoofika. Chama hicho cha PKK kisingweza kutarajia kwamba serekali ya Ujerumani ingeridhia lolote kwa ajili ya kuachiliwa huru rai zake hao. Kwa hivyo, Chama cha PKK kilikuwa hakina chaguo lengine. Hatua yeyote ambapo serekali ya Ujerumani ingewaradhia watekaji nyara hao ingemaanisha kuifanya serekali ya Berlin iweze kubinywa zaidi siku za mbele. Kufanya hivyo kungekuwa sio jambo lolote ila kuyaalika makundi ya siasa kali na jumuiya za kigaidi duniani kote kuendeleza mtindo wa kuwateka nyara watu.


Tangu mwaka 1993, chama cha PKK kimepigwa marufuku hapa Ujerumani, huko Marekani kimetangazwa zamani kuwa ni chama cha kigaidi na katika nchi za Ulaya kimepigwa mhuri huo huo. Mtu yeyote ambaye aona vingine, na kuwahesabu wapiganaji wa PKK kuwa ni waasi walio mashujaa, lazima sasa amefungua macho yake kutokana na mkasa huo wa utekaji nyara huko Ararat.


Bila ya shaka, hamna mtu anayebisha kwamba Wakurd huko Uturuki wana kibarua kigumu cha kuiondosha hali ya kuonewa na kukandamizwa na kwamba takwa lao la kuwa na utawala wao wa ndani ni la haki. Licha ya kuyakubalia baadhi ya matakwa ya Wakurd, hata hivyo, serekali ya Uturuki ina njia ndefu ya kwenda.


Lakini kwa vitendo, kama kile cha kuwateka nyara Wajerumani wapandaji milima, chama cha PKK hakitaweza kufikia hata moja ya malengo yake; kwa hakika, mambo yatakuwa kinyume na hivyo. Kinazidi kujiweka kabisa katika kona ya magaidi., kinaipoteza ile huruma iliokuwa inapata kutoka kwa watu na kinazifanya taasisis za usalama za Ujerumani kuwa rahisi kukiandama.


Licha ya kupigwa marufuku, Ujerumani bado imebakia kuwa ni eneo la kujiandaa kwa chama cha PKK pamoja na jumuiya zinazokifuata. Uchunguzi na hukumu zilizopitishwa mahakamani zinaonesha kwamba makada wa PKK wanawalazimisha Wakurd wachangie fedha kwa ajili ya chama hicho, wanawaandikisha wanachama wepya na mara nyingi wanatumia mabavu dhidi ya taasisi za Kituruki.


Kuna Wakurd laki tano hadi lakini nane wanaoishi hapa Ujerumani, wengi kuliko nchi yeyote ya Ulaya. Si chini ya 12,000 kati yao ni wanachama wa PKK au wa vikundi vinavoshirikiana na PKK. Naam, hao ni wachache tu. Serekali ya Ujerumani lazima sio tu iwalinde Wajerumani na Waturuki, lakini pia Wakurdi wengi walioko hapa nchini. Wao hawana lolote na chama hicho cha PKKKweli, kwa kuwateka nyara Wajerumani hao watatu waliokuwa wanapanda milima huko Ararat chama cha PKK kimesababisha msisimko mkubwa, lakini zaidi ni kwamba chama hicho kimeonesha kinatapatapa.