Kundi la Dola la kiislamu ladai kufanya shambulizi Kabul
10 Januari 2024Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na mlipuko ulioilenga gari moja mashariki mwa mji wa Kabul ambao umewaua watu angalau watatu katika shambulizi la pili la kundi hilo lililosababisha vifo nchini Afghanistan katika kipindi cha wiki moja.
Msemaji wa jeshi la polisi mjini Kabul Khali Zadran amesema watu watatu waliuliwa na watu wengine wanne kujeruhiwa na bomu lililokuwa limefichwa kwenye mkokoteni karibu na basi dogo mashariki mwa Kabul jana Jumanne.
Zadran ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba polisi imemtia mbaroni na inamzuilia mshukiwa mmoja aliyekiri kuhusika na shambulizi hilo.
Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na hujuma hiyo katika taarifa yake kwenye mtandao wa Telegram likisema limelipua kilipuzi kwenye gari lililokuwa likiwasafirisha wafanyakazi wa gereza la Pul-e-Charki.