1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Kuondoka kwa kikosi cha MINUSMA nchini Mali na athari zake

5 Julai 2023

Kufuatia shinikizo kutoka kwa watawala wa kijeshi wa Mali, Baraza la Usalama limeamua kuwaondoa walinda amani wote wa MINUSMA kufikia mwisho wa mwaka huu. Nini madhara yake?

https://p.dw.com/p/4TQXP
Ivorische Soldaten der UN-Friedensmission in Mali
Picha: SIA KAMBOU/AFP

Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kuwaondoa karibu askari 13,000 wa kulinda amani wa MINUSMA kufuatia ombi la serikali ya kijeshi ya Mali. Watalaamu wanahisi hatua hiyo itakuwa na athari kwa Mali, eneo la Sahel, na nchi ambazo zilipeleka wanajeshi wake nchini humo, ikiwemo Ujerumani. 

Mahusiano ya Mali na washirika wake wengi muhimu yamekuwa yakizorota tangu mapinduzi ya kijeshi ya Mei 2021, yaliyoongozwa na aliyekuwa wakati huo Makamu wa Rais wa kipindi cha mpito Kanali Assimi Goita. Mahusiano na Ufaransa yaliharibika. Paris iliwapeleka askari Mali kupambana na ugaidi na uasi wa Touareg mwaka wa 2012. Serikali ya Mali ilianza kuwatuhumu walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwa kushindwa katika majukumu yao. MINUSMA nayo ikalalamika kuhusu ukosefu wa uungaji mkono. Bamako kisha ikatafuta ushirikiano wa kijeshi na Urusi, ambayo ilipeleka mamluki wa Kundi la Wagner na wakufunzi wa kijeshi nchini humo

Mali I Referendum
Kanali Assimi Goita aliongoza mapinduzi ya kijeshi 2021Picha: Fatoma Coulibaly/REUTERS

‘Suala la mamlaka ya taifa'

Abdoulaye Sounaye ni mtaalamu kutoka taasisi ya the Leibniz-Zentrum Moderner Orient (ZMO) mjini Berlin "Naona kuwa ni jambo la kawaida kwa serikali ya Mali kudai mamlaka yake katika masuala ya usalama. hakuna anayeweza kupinga haki ya Mali katika suala hili, kwa sababu Mali ni taifa huru."

Sounaye, ambaye pia anafundisha katika Chuo Kikuu cha Abdou Moumouni mjini Niamey, ameiambia DW kuwa Mali ilikuwa hata hivyo imedhihirisha kuwa haina uwezo wa kuhakikisha ulinzi wa raia wake. Hasa katika upande wa kaskazini ambako mamluki wa Kirusi wa Kundi la Wagner wanaendesha harakati zao. Anasema kuondoka kwa MINUSMA pia kutaathiri usalama wa Mali na nchi Jirani za Sahel.

Soma pia: Ujerumani kuwaondoa askari Mali kwa utaratibu

Niagale Bagayoko, mtalaamu wa Sahel kutoka Ufaransa mwenye asili ya Mali, anasema kuondoka huko kulitokana na kuharibika kabisa kwa mahusiano ya Mali na Ufaransa.

Bagayoko anafafanua kuwa Mali imekuwa ikijiweka kwa muda kama taifa ambalo lilitaka kujitenga na mtawala wake wa zamani, Ufaransa.

Kati ya idhini na mashaka

Mali I Bamako
Wakaazi wa Bamako wana hisia mseto kuhusu MINUSMAPicha: Nicolas Remene/Le Pictorium/imago images

Wamali wana hisia mseto kuhusiana na sera ya jeshi. Kuna wanaohisi kuwa jukumu la walinda amani lilikuwa limemalizika. Wanahoji kuwa kuwasili kwa wanajeshi wa kigeni nchini humo hakukuimarisha hali kwa sababu mashambulizi ya itikadi kali yaliendelea kushuhudiwa katikati na kaskazini mwa nchi.

Lakini wakaazi wengine wa Bamako wanahofia kuwa kuondoka kwa MINUSMAhuenda kukawa na madhara kwa umma. Hasa kuhusiana na miradi yote ikiwemo ya misaada iliyoongozwa na ujumbe huo.

Usalama huenda ukazorota

Ni wasiwasi unaoungwa mkono na Ulf Laessing, mkuu wa ofisi ya Sahel ya Wakfu wa Konrad Adenauer mjini Bamako. Anasema katika upande wa kaskazini na katikati mwa nchi amekutana na watu wengi wanaounga mkono juhudi za MINUSMA.
Maelfu walipata ajira kupitia ujumbe huo, ambao pia ulijihusisha sana na sekta ya umma, kwa mfano kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa wasio na ajira. Laessing amekuwa Bamako tangu Novemba 2021 na aliweza tu kusafiri nchini humo, hasa upande wa kaskazini wenye machafuko, kwa sababu ya uwepo wa walindamani.

Mali, Gao | Bundeswehrsoldaten im UN-Einsatz
Karibu askari 1,100 wa Ujerumani lazima waondoke Mali ifikapo mwisho wa 2023Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Soma pia: Ujerumani yatoa masharti kwa wanajeshi wake kubaki Mali hadi 2024

Kuondoka kwa walinda amani pia kutaathiri kazi ya mashirika ya misaada na maendeleo ambayo yalitegemea ulinzi uliotolewa na ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa. Laessing ameiambia DW kuwa hali ya usalama kwa wakaazi hakika itakuwa mbaya.

Kwa mujibu wa mtalaamu huyo, serikali ya Mali itajaribu kujaza ombwe lililowekwa na MINUSMA kwa kutumia washirika wake wa Urusi. "Jeshi limefanya ununuzi mkubwa: helikopta mpya, ndege za kivita na silaha nyingine. Sasa watajaribu kuijaza nafasi ya MINUSMA. Makundi yenye silaha, majihadi, hakika pia yatajaribu kulitumia ombwe hilo kwa manufaa yao."

Zaidi ya askari 13,000 na maafisa wa polisi, Pamoja na vifaa vyao – ikiwemo helikopta na magari ya kivita – wanapaswa kujipanga na kuondoka. Miongoni mwao ni wanajeshi 1,100 wa Ujerumani. Maelfu ya Wamali wameuawa katika mizozo kote nchini humo. Katika miezi ya karibuni, zaidi ya askari 300 wa kulinda amani walipoteza maisha yao nchini Mali.