1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

''Kura ya maoni" kukamilika kwenye maeneo ya Ukraine

27 Septemba 2022

Kile kinachoitwa kura za maoni zilizoandaliwa na Urusi kwenye majimbo manne ya Ukraine yanayodhibitiwa na vikosi vya Urusi zinatarajiwa kumalizika Jumanne.

https://p.dw.com/p/4HOs0
Ukraine | Krieg | Scheinreferenden
Picha: ITAR-TASS/IMAGO

Ukraine pamoja na washirika wake zimekosoa vikali kile ambacho Urusi inakiita kura za maoni kwenye maeneo ya majimbo ya Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhzhya, wakisema zinakiuka sheria ya kimataifa. Watu kwenye majimbo hayo yanayodhibitiwa na Urusi watakuwa na muda wa hadi saa kumi kamili Jumanne jioni kupiga kura zao za kuamua kujiunga na Shirikisho la Urusi.

Putin kuimarisha mamlaka yake kusini na mashariki mwa Ukraine

Ikiwa ni takribani miezi saba tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, mwezi huu vikosi vya Urusi vimekabiliwa na mashambulizi makali kwenye maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine, ambayo waangalizi wanasema ndiyo sababu iliyomsukuma Rais Vladmir Putin kuharakisha kuandaa kile kinachoitwa kura za maoni ili kuimarisha mamlaka ya Urusi kwenye maeneo hayo.

Kwa siku kadhaa televisheni ya taifa ya Urusi imewaonesha watu kwenye maeneo yanayodhibitiwa wakielezea furaha yao kwamba hivi karibuni watakuwa sehemu ya Urusi. Kinyume chake, vyombo huru vya habari vinaripoti kuwa watu wanapiga kura kwa shinikizo, huku wakiwa wameelekezewa mtutu wa bunduki.

Ukraine, Lugansk | Start des Scheinreferendums
Masanduku ya kura katika kituo kimoja katika jimbo la LuhanskPicha: Dmitry Rogulin/TASS/dpa/picture alliance

Hata hivyo, kwenye jimbo la Luhansk, maafisa wameripoti kuwepo mashambulizi kadhaa ya roketi kwenye mji wa Alchevsk, lakini vituo vyote vya kupigia kura kwenye eneo hilo viko wazi.

Kura hiyo ya kuunga mkono kujiunga na Shirikisho la Urusi inatarajiwa kupita kwa asilimia 80 hadi 90. Baada ya hapo, viongozi wa majimbo yanayotaka kujitenga wanakusudia kutuma maombi rasmi kwa Rais Putin kwa ajili ya kuandikishwa kuwa sehemu ya eneo la Urusi.

Ukraine: Watakaoisaidia Urusi kushtakiwa kwa uhaini

Wakati huo huo, mshauri wa Rais wa Ukraine, Mikhailo Podolyak amesema wananchi wa Ukraine watakaoisaidia kile kinachoitwa kura za maoni zinazoungwa mkono na Urusi, watakabiliwa na mashtaka ya uhaini na kufungwa miaka ipatayo mitano gerezani.

"Tuna orodha ya majina ya watu ambao wamehusika kwa njia fulani. Lakini wananchi wa Ukraine ambao wamelazimishwa kupiga kura, hawatoshitakiwa," alifafanua Podolyak.

Katika mahojiano yake na gazeti la Uswisi la Blick, Podolyak amesema masanduku ya kura yanasambazwa nyumba hadi nyumba na wakaazi wanalazimishwa kupiga kura mbele ya vikosi vya usalama.

Hayo yanajiri wakati ambapo Rais Putin ametishia kutumia silaha za nyuklia ili kuilinda ardhi ya Urusi, ambayo itayajumuisha majimbo hayo manne ya Ukraine kwa lengo la kuizuia Ukraine kujaribu kuyakomboa majimbo hayo.

Pia Putin ametangaza kuwa Urusi inawaita askari 300,000 wa akiba, hatua ambayo imesababisha baadhi ya wanaume wa Urusi wanaohofia kupelekwa Ukraine, kukimbilia kwenye nchi za jirani.

London | James Cleverly Staatsminister für den Nahen Osten und Nordafrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, James Cleverly Picha: Justin Ng/Avalon/Photoshot/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, Uingereza imetangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi kutokana na kura hiyo kwenye majimbo ya Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, James Cleverly amesema kura hizo zilizopigwa kwa mtutu wa bunduki haziwezi kuwa huru au za haki na kamwe matokeo yake hayatotambuliwa.

Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Ufaransa ziarani Kiev

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna yuko mjini Kiev, katika ziara ambayo haikutangazwa, kwa lengo ya kuonesha mshikamano na nchi hiyo iliyovamiwa na Urusi.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema nchi yake itatoa dola milioni 457.5 kama msaada wa usalama wa raia nchini Ukraine. Msaada huo mpya utakuwa kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa sheria na vyombo vya kusimamia haki, pamoja na kusaidia katika kuchunguza madai ya ukatili uliofanywa na vikosi vya Urusi.

(AFP, DPA, AP, Reuters, DW https://bit.ly/3fpfzBS)