1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kurdistan kupeleka wapiganaji Kobane

Mohammed Khelef22 Oktoba 2014

Bunge la Kurdistan linapiga kura kuviruhusu vikosi vyake kwenda Syria kuwasaidia Wakurdi wanaopambana na wapiganaji wa Dola la Kiislamu, huku mapambano makali yakiendelea mjini Kobane na vitongoji vyake.

https://p.dw.com/p/1DZfs
Moshi ukifuka kutoka mji wa Kobane nchini Syria.
Moshi ukifuka kutoka mji wa Kobane nchini Syria.Picha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Kwa mujibu wa mkuu wa chama Kurdistan Democrats, Omid Khoshnaw, kura ya leo (22 Oktoba) ni ya kumpa mamlaka Rais Masoud Barzani wa Kurdistan kutuma wanajeshi kwenye mji wa Kobane, na kama itapitishwa na bunge la jimbo hilo linalojumuisha mikoa mitatu na lenye mamlaka makubwa ya ndani, utakuwa ni uamuzi wa kwanza wa kutuma wanajeshi bila ya kuishirikisha serikali kuu mjini Baghdad.

Tangu kuibuka na kupanda kwa kasi nguvu ya kundi la IS, ni vikosi vya Kikurdi ndivyo vilivyoonesha uthubutu zaidi wa kukabiliana nao kaskazini mwa Iraq kuliko hata jeshi rasmi la nchi hiyo iliyolemazwa na mgogoro wa kimadhehebu kati ya Sunni na Shia.

Bado Iraq haijasema kitu kuhusu kura hiyo, na Waziri wake Mkuu, Haidar Abadi, yuko mjini Tehran, Iran, ambako Rais wa nchi hiyo, Hassan Rouhani, amemuhakikishia kuendelea kumuunga mkono kwenye vita dhidi ya IS, tena bila ya masharti yoyote. Hii ni ziara ya kwanza ya Abadi nchini Iran tangu ashikilie wadhifa huo mwezi uliopita.

Wanajeshi wa Uturuki katika upande wa pili wa mji wa Kobane.
Wanajeshi wa Uturuki katika upande wa pili wa mji wa Kobane.Picha: picture-alliance/AA/M. Kula

Mapigano yaendelea Kobane

Katika mji wa Kobane nchini Syria, hali inaendelea kuwa ya mashaka baada ya mashambulizi makali yaliyofanywa na wapiganaji wa IS ndani ya masaa 48 yaliyopita, yakiwemo yale ya waripuaji wa kujitoa muhanga.

Upande wa mashariki mwa mji huo, wanamgambo wa IS wamekabiliana na wapiganaji wa Kikurdi, ambako kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria, wapiganaji 30 wa IS na 11 wa Kikurdi wameuawa.

Shirika hilo lenye makao yake London, linasema kuna taarifa za IS kuongeza wapiganaji na vifaa vya kivita kwenye eneo hilo, baada ya kuelekea kushindwa.

Silaha za Marekani zaangukiwa kwa IS

Wakati hayo yakiendelea, sehemu ya shehena ya silaha zilizodondoshwa na ndege za Marekani kwa ajili ya wapiganaji wa Kikurdi imeripotiwa kuangukia mikononi mwa IS. Picha za vidio zilizorushwa mtandaoni hapo jana, zinawaonesha wapiganaji hao wakiwa na masanduku yenye mabomu, bunduki na risasi kutoka ndege za Marekani.

Makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, yamethibitisha tukio hilo, ambalo huenda likahisabika kuwa mapungufu makubwa kwenye mkakati wa vita vya kimataifa dhidi ya IS vinavyoongozwa na Marekani.

Wakimbizi wa Kobane kwenye kambi za Uturuki.
Wakimbizi wa Kobane kwenye kambi za Uturuki.Picha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Hapa Ujerumani, mamlaka za uwanja wa ndege mjini Frankfurt zimethibitisha kuwakamata wasichana watatu raia wa Marekani, wanaohofiwa kuwa walikuwa njiani kuelekea Syria, kujiunga na kundi la IS, kupitia Uturuki.

Wasichana hao, wawili wakiwa mtu na dada yake - wenye umri wa miaka 15 na 17 - na mwengine mwenye umri wa miaka 16, wanatokea jimbo la Denver, na mamlaka za jimbo hilo zimethibitisha kuwa tayari wameshakabidhiwa kwao.

Wasichana hao wenye asili za Somalia na Sudan, walikamatwa juzi Jumapili na polisi wa mpakani, ambapo vyombo vya habari vya Marekani vilitangaza hapo jana kuwa walikuwa njiani kuelekea Syria.

Wapiganaji kadhaa wa kundi la IS wanaaminika kutokea mataifa ya Magharibi, ambapo mataifa hayo sasa yanahofia watarejea kufanya mashambulizi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/dpa
Mhariri: Mohamed Abdulrahman