Kushner akutana na Netanyahu na Abbas
25 Agosti 2017Ziara hiyo inafanyika huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas, wakiwa na matumaini madogo ya kufanikiwa kwa mchakato mpya wa amani. Netanyahu ambaye jana alikutana na Kushner mjini Jerusalem, amesema walikuwa na mambo mengi ya kujadili, ikiwemo hatua ya kuelekea katika amani, utulivu, usalama na ustawi katika Mashariki ya Kati.
''Nina furaha sana kukuona tena Jared na ujumbe wako na juhudi ambazo unaziongoza kwa niaba ya rais. Nadhani hii ni ishara ya ushirikiano mkubwa kati yetu na malengo makuu ambayo yanatuongoza,'' alisema Netanyahu. Amebainisha kuwa ana uhakika masuala yote hayo yatakuwa ndani ya uwezo wao.
Kwa upande wake Kushner, ambaye ni mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani, amesema kiongozi huyo wa Marekani amejizatiti sana kufikia suluhu ambayo itafanikisha kuleta ustawi na amani katika eneo la Mashariki ya Kati. Baadae ofisi ya Netanyahu iliyaelezea mazungumzo hayo kama ya ''kujenga na muhimu'', ingawa haikutoa taarifa zaidi.
Hata hivyo, Nabil Abu Rdeneh, msemaji wa kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas, amesema haikufahamika wazi iwapo Kushner alikuwa muwazi wakati wa mazungumzo yake na Abbas ambayo yalidumu kwa saa tatu, ingawa amesema mazungumzo hayo yalikuwa yenye manufaa.
Mazungumzo ya amani ni njia ya kusonga mbele
Muda mchache baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Ramallah, Ikulu ya Marekani ilisema pande zote mbili zimekubali kwamba mazungumzo ya amani ya Israel na Palestina yatakayosimamiwa na Marekani ni njia imara ya kusonga mbele.
Kabla ya mkutano wake na Kushner, Abbas alisema kuwa nchi yake inathamini sana juhudi zinazofanywa na Rais Trump. ''Tumethibitisha kuwa ujumbe huu unafanya kazi kuelekea katika amani na tutashirikiana nao kufikia haraka kile ambacho Rais Trump amekiita kuwa ni mpango wa amani. Tunafahamu kwamba mambo ni magumu na yanachanganya, lakini hakuna kisichowezakana kama mtu una nia njema,'' alisema Abbas.
Awali, wananchi wa Palestina walifurahishwa na hatua ya kuchaguliwa Trump kuiongoza Marekani, lakini tangu wakati huo wamekatishwa tamaa na kile wanachosema ni kushindwa kwa kiongozi huyo kuwasilisha mpango wa amani. Wapalestina wanataka Israel isitishe ujenzi wa makaazi katika ardhi ambayo inaikalia kwa mabavu na kujitolea kwa Marekani katika kuundwa dola la Wapalestina, kama sehemu ya mpango wa kupatikana amani kati yake na Israel.
Katika ziara yake hiyo, Kushner ameongozana na mjumbe wa Marekani kwa ajili ya mazungumzo ya kimataifa, Jason Greenblatt, na naibu mshauri wa usalama wa taifa, Dina Powell. Ujumbe huo pia ulikutana na maafisa wa Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Jordan. Kushner anatarajiwa kurejea Marekani leo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Mohammed Khelef