1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umuhimu wa mkuu wa jeshi la Pakistan kwa taifa hilo

25 Novemba 2022

Pakistan imemtaja Luteni Jenerali Asim Munir kama mkuu wa jeshi lenye silaha za nyuklia wa nchi hiyo, taasisi yenye nguvu zaidi katika taifa ambalo haliishiwi na migogoro.

https://p.dw.com/p/4K53y
Pakistan | General Syed Asim Muni
Picha: W.K. Yousufzai/AP/picture alliance

Uteuzi huo unaweza kuwa na athari kubwa kwa siku zijazo kwa demokrasia tete ya Pakistan, na kama mahusiano na nchi jirani ya India yanaweza kuimarika.

Nafasi ya jeshi nchini Pakistan

Katika kipindi cha miaka 75 tangu uhuru na kuundwa kwa Pakistan baada ya kutenganishwa na India, jeshi limechukuwa kwa nguvu madaraka mara tatu na kulitawala moja kwa moja taifa hilo la Kiislamu kwa zaidi ya miongo mitatu pamoja na kupigana vita mara tatu na India.

Hata serikali ya kiraia inaposhika madaraka, majenerali wa Pakistan wanakuwa na ushawishi mkubwa juu ya masuala ya usalama na mambo ya nje.

Aaim Munir ni nani?

Munir atachukua nafasi ya Jenerali Qamar Javed Bajwa, ambaye anastaafu

baadaye mwezi huu baada ya kuhudumu kwa miaka sita.

Munir alihudumu katika eneo linalozozaniwa na India ambalo linapakana na China na pia Saudi Arabia, ambayo ndio mfadhili mkuu wa kifedha wa Pakistan.

Baadaye aliongoza mashirika mawili ya kijasusi yenye ushawishi mkubwa nchini Pakistan ambayo ni Shirika la Ujasusi la Jeshi (MI) mwaka 2017 na lililokuwa Shirika la Huduma za Kijasusi (ISI) mwaka 2018.

Aliondolewa kama mkuu wa ISI baada ya miezi minane tu kwa ombi la waziri mkuu wa wakati huo, Imran Khan. Hakuna sababu iliyotolewa ya kuondolewa kwake

Kwanini ni muhimu duniani

Mkuu wa jeshi la Pakistan atachukua jukumu muhimu katika kudhibiti hatari

za mzozo na taifa pinzani la India lenye silaha za nyuklia katika mpaka wake wa mashariki, huku akikabiliana na ukosefu wa utulivu na uwezekano wa msuguano na Afghanistan kwenye mpaka wake wa magharibi.

Videostill | DW News | Imran Khan
Imran Khan - Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan

Mataifa mengi makubwa duniani, ikiwa ni pamoja na Marekani na China, yana

uhusiano wa moja kwa moja na jeshi la Pakistan, kwa kuzingatia nchi hiyo ni eneo la kimkakati katika ukanda tete wa pwani karibu na njia kuu za meli zinazohudumia eneo tajiri la Ghuba lenye mafuta mengi.

Mara kwa mara, serikali za kigeni zimetilia shaka usalama wa silaha za nyuklia zinazojumuisha makombora ya masafa marefu katika taifa ambalo mara kwa mara linahitaji msaada kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) na ambapo makundi ya wapiganaji wanaopinga mataifa ya Magharibi na India yameongezeka

Na usalama wa ndani umekuwa shida ya mara kwa mara kwa sababu ya uasi katika maeneo ya makabila ya Pashtun na Baloch.

Licha ya hatari zote, Pakistan na jeshi lake wamepuuzilia mbali wasiwasi wa mataifa ya kigeni kuhusu udhibiti na usalama wa silaha zake za nyuklia.

Kwanini uteuzi huu ni muhimu ndani ya nchi

Jeshi kwa muda mrefu limekuwa likishutumiwa kwa kuhujumu mchakato wa kidemokrasia ili kudumisha madaraka wake. Mawaziri wakuu kumi na tisa walichaguliwa, lakini hakuna hata mmoja aliyemaliza muda wao wa miaka mitano.

Baada ya kukiri hivi karibuni kujihusisha na siasa, katika siku za nyuma, jeshi limesema halitaingilia tena. Iwapo kiongozi huyo mpya atazingatia ahadi hiyo,  inaweza kuwa muhimu kwa mageuzi ya kidemokrasia ya Pakistan.

Pakistan iko katika hali nyingine na kutokuwa na uhakika wa kisiasa, kwani Khan anaongoza maandamano ya nchi nzima katika jaribio la kumlazimisha Waziri Mkuu Shehbaz Sharif katika uchaguzi wa mapema.

Mkuu huyo mpya wa jeshi anayeingia, anaweza kutekeleza jukumu muhimu katika kupunguza joto la kisiasa wakati Pakistan inapojaribu kupambana na mgogoro wa kiuchumi na pia athari za mafuriko makubwa kuwahi kutokezea nchini humo.

Urithi wa Bajwa

Bajwa alitaka kusawazisha uhusiano na China na Marekani. Wakati Pakistan ilipojisogeza karibu na China, Bajwa pia alifanya kazi kurekebisha uhusiano na Marekani ambayo alifanya nayo kazi kwa karibu wakati wa kuhamisha watu kutoka Kabul mnamo 2021 wakati vikosi vya Magharibi vilipoondoka Afghanistan.